Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
BONDIA wa Tanzania Selemani Kidunda amesema Mpinzani wake Erick Tshimanga Katompa alidhamiria kumpiga kichwa kama alivyokua ameahidi.
Kidunda amesema hayo baada ya pambano lao la kuwania mkanda wa WBF kati ya Suleiman Kidunda na Erick Tshimanga Katompa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kushindwa kumalizika katika raundi ya tatu.
Hatua hiyo ilikuja baada ya wawili hao kugongana na Kidunda kuchanika juu ya jicho na daktari kusema hataweza kuendelea na mwamuzi wa pambano hilo kuamuru mchezo uishie hapo.
Bondia Selemani Kidunda amesema tayari alikua na uhakika wa kushinda sababu alishamkalisha katika Raundi zote za mwanzo ila Katompa alifanya faulo ile ya kumpiga kichwa kama alivyoahidi.
Pambano hilo lililosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mchezo wa ngumi lilifanyika ukumbi wa Ubungo wa Plazza Jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.
Wakitumia sheria za WBF baada ya bondia Mtanzania, Kidunda kuchanika juu ya jicho kufuatia kugongwa kichwa na Katompa mwanzoni mwa Raundi ya nne, majaji waliamua kutoa droo.
Hata hivyo, majaji waliweka wazi hadi pambano hilo la uzito wa Middle kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF, Kdunda alikuwa anaongoza kwa pointi.
Ikumbukwe, Katompa alimtwanga kwa KO Mtanzania mwingine, Abdallah Shaabani Pazi 'Dullah Mbabe' Oktoba 9 mwaka jana ukumbi wa PTA, Temeke JijininDar es Salaam na jana Kidunda alipewa nafasi kubwa ya kumlipia kisasi Mtanzania mwenzake.
Muandaaji wa Pambano hilo,Kapten Selemani Semunyu amesema amesema shughuli imeshaisha na nataka nione mapambano mengine makubwa kwa mabondia wetu.
Amesema, katika raundi zote walizocheza kabla ya Pambano kuhairishwa Kidunda alikua anaongoza na kwahiyo Kumaliza sare ina maana uwiano wa katompa na kidunda uko sawa.
Semunyu amewaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono, mashabiki wa ngumi ni wengi sana na sasa hivi tuangalie mbele zaidi kwa kuandaa mapambano makubwa na kuleta mabondia bora.
Mapambano mengine ya jana Mtanzania, Ismail Galiatano alishinda kwa pointi dhidi ya Denis Mwale wa Malawi kwenye pambano la nane na kutwaa taji la P.S.T uzito wa Super Bantam.
Mtanzania, mwingine, George Bonabucha alimshinda kwa pointi Mzimbabwe, Hassan Milanzi kwenye na kutwaa pia mkanda wa P.S.T, wakati Grace Mwakamele alikuwa Mtanzania pekee aliyepoteza pambano usiku huo baada ya kushindwa kwa pointi na Mmalawi, Ruth Chisale aliyejinyakulia taji la PST pia.
Oscar Richard pia alibeba mkanda wa PST baada ya kumtwanga Paul Magesta, Ibrahim CMgendera 'Ibrah Class alikalisha Kelvin Majiba kwa Knockout (KO).
Juma Choki alimkalisha kwa KO, Salim Chazama kutoka Malawi, Vigulo Shafi akamshinda kwa pointi Ally Kilongola na Mwanajeshi mwingine, Haruna Swanga akamshinda Daniel Matefu kwa KO kwenye pambano la tano lenye raundi nne.
Iddi Jumanne alimchapa Hamis Kibodi kwa pointi , Joseph Mchapeni alimkalisha Paschal Goba kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya raundi ya pili, Najma Isike akashinda kwa pointi dhidi ya Leila Yazidu na King Makassy alimshinda kwa pointi Ibrahim Mpili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...