Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) limezindua kampeni yake kabambe inayoitwa “WESE NDIO MCHONGO” inayotoa fursa kwa wateja wake kote nchini kujaziwa mafuta kwenye vyombo vyao usafiri, ikiwa ni zawadi kwa wateja wa shirika hilo katika kuadhimisha ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya miezi mitatu uliofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya wiki Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji wa Shirika hilo Bw Mohammedi Ameir alisema kampeni hiyo inawalenga wateja wa Bima Kubwa ya vyombo vya moto ambapo kila mteja ataekakata bima hiyo atakuwa kwenye nafasi ya kujipatia mafuta kwa ajili ya chombo chake cha usafiri.

“Shirika la Bima Zanzibar ni shirika ambalo linawateja wengi kutoka pande zote kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar na siku zote tumekuwa karibu zaidi na wateja wetu. Kwa kuliona hilo tumeona katika kipindi hiki ambacho tunasherehekea maadhimisho haya muhimu kitaifa kwa pande zote mbili ni vema tuje na zawadi hii kwa wateja wetu.

“Pamoja na maadhimisho haya tunaamini washindi wetu wataweza kutumia zawadi hii ya mafuta kuokoa fedha ambayo wataitumia kwenye matumizi yao mengine ya mwisho wa mwaka ambao huwa unaambatana na sikukuu pamoja na mahitaji ya shule kwa watoto,’’ alisema.

Akizungumza zaidi kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Kituo cha Mauzo ZIC tawi Posta Mpya jijini Dar es Salaam Bi Amina Mohammed alisema ili mteja aingie katika droo ya kujaziwa mafuta ni lazima afike katika ofisi za shirika hilo zilizopo kote nchini kwaajili ya kukata bima kubwa ambayo itamuwezesha yeye kupata bahati ya kujaziwa mafuta kuanzia lita tatu (3) hadi lita mia moja (100).’’

“Kitakachoamua kiasi cha mafuta anachostahili kupatiwa mteja ni bahati yake katika kuchagua kimpira kidogo (ball) chenye karatasi ndani iliyoandikwa kiasi cha mafuta aliyoshinda ili aweze kupatiwa mafuta yake kupitia vituo mbambalimbali vya mafuta kokote alipo nchini,’’ alisema.

Kampeni hiyo itadumu kwa muda wa miezi mitatu, ikilenga kuwafikia wateja wote wa shirika la Bima Zanzibar waliopo Tanzania Nzima, ikiwa na kauli mbiu “Wese Ndio Mchongo, Kata Bima Tukajaze Wese”.

Maofisa wa Shirika la Bima Zanzibar wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji wa Shirika hilo Bw Mohammedi Ameir (wa pili kushoto) wakiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mipira maalumu iliyohifadhi namba tofauti za kiasi cha mafuta kitakachotolewa kwa washindi wa kampeni ya “Wese Ndio Mchongo” inayotoa fursa kwa wateja wa shirika hilo kote nchini kujaziwa mafuta kwenye vyombo vyao usafiri  ikiwa ni zawadi kwao katika kuadhimisha ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Kituo cha Mauzo ZIC tawi Posta Mpya jijini Dar es Salaam Bi Amina Mohammed (Kushoto), Ofisa uwekezaji na maendeleo ya Biashara ZIC Bw Rahim Hamza (Kulia) na Kaimu Meneja wa Tawi tawi ZIC Posta Mpya jijini Dar es Salaam Bi Fatma Hadji (wa pili kulia)

Kaimu Meneja wa Tawi Shirika la Bima Zanzibar ZIC Posta Mpya jijini Dar es Salaam Bi Fatma Hadji (wa pili kulia) wakiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mfano wa karatasi yenye namba inayoashiria kiasi cha mafuta kitakachotolewa kwa washindi wa kampeni ya “Wese Ndio Mchongo” inayotoa fursa kwa wateja wa shirika hilo kote nchini kujaziwa mafuta kwenye vyombo vyao usafiri  ikiwa ni zawadi kwao katika kuadhimisha ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji wa Shirika hilo Bw Mohammedi Ameir (wa pili kushoto), Mkuu wa Kituo cha Mauzo ZIC tawi Posta Mpya jijini Dar es Salaam Bi Amina Mohammed (Kushoto) na  Ofisa uwekezaji na maendeleo ya Biashara ZIC Bw Rahim Hamza (Kulia)

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...