Katika kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Ubalozi wa Tanzania nchini Israel uliandaa na kudhamini mashindano ya mchezo wa gofu ambao ulishirikisha wachezaji 70, tarehe 7 Disemba 2021, katika viwanja vya Klabu ya Gofu ya Caesaria. 


Mashindano hayo yalizinduliwa rasmi na Mhe. Job Daudi Masima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Israel. Katika hotuba yake fupi ya uzinduzi, Mhe. Masima, alieleza kuwa mashindano hayo yameandaliwa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.

 

Mashindano hayo yalifuatiwa na hafla ya usiku iliyofanyika katika Ukumbi wa Amphorae Winery, ulioko Kerem Maharal ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Issawi Frej, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Taifa la Israel. 

Katika hotuba yake, Mhe. Masima alielezea mafanikio yaliyopatikana na changamoto ambazo Tanzania Bara imekabiliana nazo tangu ipate uhuru mpaka sasa. Miongoni mwa mafanikio hayo ni amani na utulivu, umoja kupitia lugha ya Kiswahili na maendeleo ya miundombinu mbalimbali ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, treni ya mwendokasi na mtandao wa barabara nchini.

 

Wakati wa hafla hiyo washindi watatu wa mashindano ya gofu walikabidhiwa vikombe na Mhe. Mgeni Rasmi wakati washiriki wote walipewa zawadi kutambua ushiriki wao. Vilevile, ilichezeshwa bahati nasibu kwa washiriki wote wa shindano la gofu ambapo mshindi wa kwanza alijinyakulia zawadi ya kutembelea mbuga za wanyama na vivutio vya utalii Zanzibar kwa muda wa wiki moja, tiketi ya ndege na mwenza wake na kulipiwa usafiri wa ndani na malazi; mshindi wa pili alijinyakulia zawadi ya kutembelea mbuga za wanyama kwa muda wa wiki moja na kulipiwa usafiri wa ndani na malazi; na mshindi wa tatu alijinyakulia zawadi ya kutembelea vivutio vya utalii Zanzibar kwa muda wa wiki moja na kulipiwa usafiri wa ndani na malazi. Hafla ilihitimishwa kwa Mgeni Rasmi na baadhi ya waalikwa wakiwemo washindi wa gofu na bahati nasibu kukabidhiwa zawadi ya vitabu vya “Jifunze Kiswahili”.

 

Mhe. Masima atafanya mahojiano na runinga ya i24 News Israel mojawapo ya vyombo vya habari vikubwa nchini hapa, tarehe 9 Disemba kwenye kilele cha maadhimisho hayo. Makala mbalimbali kuhusu Tanzania zimeandikwa kwenye magazeti kama Jerusalem Post na mitandao yenye wasomaji wengi nchini hapa kama Israel Hayom Online. 

 

Tarehe 10 Disemba 2021, Mhe. Masima anatarajiwa kuzindua rasmi matangazo ya vivutio vya utalii vya Tanzania yatakayobandikwa kwenye mabasi makubwa yanayofanya safari katika jiji la Tel Aviv na miji ya jirani, kwa muda wa wiki tatu.

 


















 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...