Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma.
Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.

Na. James K. Mwanamyoto-Kigoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatowasaliti katika kutetea stahiki zao Watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa lao.

Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Mchengerwa amesema atahakikisha anasimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma nchini kwa lengo la kuwaongezea morali ya utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.

Kufuatia uamuzi wake wa kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kufanya kazi kwa mazoea kwani wasipowajibika hatokuwa tayari kutetea stahiki zao.

“Pale ambapo tutabaini kuna mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitokuwa tayari kumtetea lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote mwadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa taifa lake muda wote asubuhi, mchana, jioni na usiku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewaelekeza watendaji kufuatilia utendaji kazi wa watumishi walio chini yao mara kwa mara na kumtaka kila mtumishi kuongeza ubunifu katika eneo lake la kazi ili aweze kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri kutenga bajeti ya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma walio katika maeneo yao ili waweze kuwa na weledi, ubunifu na kuongeza ufanisi kiutendaji.

Waziri Mchengerwa yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...