Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kushoto) akikabidhi mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Msanda Muungano wilaya ya Sumbawanga kwa Mkurugenzi wa kampuni ya ukandarasi ya Kiluswa Buliding Contrators Anyosisye Kiluswa leo hafla iliyofanyika mjini Sumbawanga.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boaz Matundali akisaini moja ya mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya RUWASA na wakandarasi leo mjini Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na wakandarasi wa miradi ya maji leo Ofisini kwake Sumbawanga ambapo amewataka wakatekeleze miradi hiyo kwa uadilifu na uzalendo ili kero ya upatikanaji vijijini imalizike. Jumla ya miakaba minne yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.23 imesainiwa leo kati ya RUWASA Rukwa na wakandarasi wazawa.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)


WAKANDARASI wanaotekeleza miradi ya maji mkoani Rukwa wametakiwa kuwa waadilifu na wazalendo ili wananchi wapate maji vijijini na mijini kwa ustawi wa jamii hatua itakayo ondoa kero za ukosefu wa maji.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati aliposhuhudia hafla ya utiaji saini mikataba minne ya miradi ya maji kwa kati ya Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na wakandarasi mjini Sumbawanga.

“Miradi hii haihitaji stori, tunahitaji siku 180 za mkataba zitumike kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji huku tukizingatia matumizi sahihi ya fedha pamoja na uadilifu “alisema Mkirikiti.

Katika hafla hiyo mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi 1,383,238,518 itakayotekelezwa kwa siku 180 katika wilaya za Nkasi na Sumbawanga.

Akitoa taarifa kabla ya utiaji saini, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Boaz Matundali alisema jumla ya miradi 19 imetangazwa katika mwaka huu wa fedha ambapo minne kati yake imepata wakandarasi.

Mhandisi Boaz alitaja miradi itakayosainiwa kuwa ni ujenzi wa mradi wa maji Msanda Muungano wilaya ya Sumbawanga wenye thamani ya shilingi Milioni 295.7 chini ya mkandarasi Kiluswa Building Contrators ya Sumbawanga.

Miradi mengine itatekelezwa katika wilaya ya Nkasi ambayo ni ujenzi wa mradi wa maji Lyazumbi (shilingi Milioni 308.4), ujenzi wa mradi wa maji Kacheche (shilingi Milioni 385.0) na mradi wa maji Masolo (shilingi Milioni 395.9) yote itatekelezwa na mkandarasi Consel Construction and Engineering Services ya Mwanza.

Katika hatua nyingine Mhandisi Boaz alisema katika mwaka huu RUWASA mkoa wa Rukwa unatumia wakandarasi katika kutekeleza miradi yake tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita ambapo miradi ilitumia force account na nguvu za wananchi hivyo wanategemea itakamilika ndani ya kipindi cha siku 180 za mkataba.

“Kukamilika kwa miradi hii minne kutasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji maji mkoa wa Rukwa toka asilimia 64 za sasa hadi kufikia asilimia 67 kwenye vijiji “alisisitiza Mhandisi Boaz.

Kwa upande wake mwakilishi wa wakandarasi Anyosisye Kiluswa aliishukuru serikali kwa kutoa kazi hizo kwa wakandarasi wazawa hatua itakayosaidia kukuza biashara na kuchangia upatikanaji ajira.

Kiluswa alitoa ahadi kuwa miradi hiyo wataitekeleza kwa ufanisi na ubora ili kuwezesha wananchi kupata maji kama serikali ilivyokusudia.

Naye Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Thomas Msuta alisema wanafuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inakuwepo kwenye miradi hiyo.

“Sisi TAKUKURU tutafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii ili fedha za serikali zitumike kwa usahihi kuhakikisha lengo la kuwezesha wananchi kupata maji “alisisitiza Msuta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...