Jumla ya watoto 23 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo (Congenital Heart Disease) wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Upasuaji huo wa moyo unafanywa na Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saud Arabia.

Matibabu yanayotolewa katika kambi hii ni kuziba matundu ndani ya moyo, kuzibua njia za mishipa ya damu ya moyo iliyobana, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo iliyokaa vibaya na kuzifanyia marekebisho Valvu za moyo kwa kuzikarabati au kubadilisha kabisa na kuweka za chuma. Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri.

Hii ni mara ya pili kwa wataalamu hawa kuja katika Taasisi yetu kwa ajili ya kufanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto. Mara ya mwisho walikuja mwaka 2019 kabla ya janga la ugonjwa wa UVIKO – 19 lililozuia ujio wao kwa mwaka 2020. Wataalamu hawa wamepongeza jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu katika kipindi cha miaka miwili ambacho hawakupata nafasi ya kuja nchini.Pia wamewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kuongeza ujuzi wa kufanya upasuaji wa moyo.

Kambi hii ya siku 10 ambayo inaenda sambamba na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wataalamu wetu wa kitanzania na wageni ilianza tarehe 11/12/2021 na itamalizika tarehe 20/12/2021.

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saud Arabia wakimfanyia mtoto upasuaji mkubwa wa moyo wa kuziba tundu lililopo kwenye  moyo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya watoto 23 wameshafanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na hali zao zinaendelea vizuri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...