Adeladius Makwega,Dodoma

Siku hiyo nilipigiwa simu na mkuu wangu juu ya kushiriki kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Zimamoto Jijini Dodoma. Nilitoka kwangu Chamwino na kupanda daladala hadi Jijini Dodoma ambapo ni mwendo wa saa nzima. Nilishuka Kimbinyiko, kuvuka barabara , kupitia kandokando ya shule ya Sekondari Dodoma, nilifika Barabara ya Makole kuelekea Jengo la Zimamoto.

Nilipofika hapo niliwauliza Askari wa Zimamoto pahala panapofanyika mkutano huo, walinielekeza vizuri. Maelekezo ya Askari wa Zimamoto yalinipa picha namna Askari wa Zimamoto walivyo tofauti na Askari wengine.

“Mzee pita hapa, utakutana na magari yenye namba za Zanzibar, panda ngazi na ghorofa ya pili utakutana na bango la mkutano huo. Kwani mzee unajua kusoma? Afande mpeleke mgeni huyu.” Nilipatiwa Askari wakike, muda huo huo kabla sijajibu najua kusoma au la.

Niliamini kuwa ni kweli Jeshi la Zimamoto ni mabingwa wa kupambana na majanga hasa hasa wakipatiwa vifaa bora. Kumbuka kuwa sasa naenda ukumbini na Askari wa Zimamoto aliyekuwa ananiongoza, alikuwa binti mrembo, nadhani ndiyo kwanza alikuwa ameanza kazi, hilo nilibaini kwa kumtazama tu, huku akiwa amevalia rasmi sare zake zilizomkaa vizuri, kwa maana alivaa akavalika kweli kweli. Nilipomuuliza anatokea mkoa gani? alinijibu kuwa anatokea huko Lindi. Niliomba namba yake ya simu maana nyumbani kwetu kuna vijana wa kiume wengi, nilitamani sana kijana mmoja wa kwetu atufungishe safari hadi Lindi tukapose binti huyo ili aje kwetu Mbagala kutusaidia kupambana na majanga.Maana nyumbani kwetu Mbagala nyumba zetu zimekaa shaghalabagala hata moto ukitokea ni tabu sana.

Nilipofika ukumbi Askari huyu wa Zimamoto alirudi zake na mie kuingia kikaoni, kikao kiliwahusu baadhi ya viongozi wa taasisi za Zanzibar na zile za Tanganyika.

Nikiwa katika kikao hicho, ilibainika kuwa Mwendesha Ratiba (MC)alichelewa mie niliombwa kuokoa jahazi.
Niliwaza moyoni kuwa pale unapoambiwa kufanya jambo la jamii wewe kuwa tayari kwa kazi hiyo, niliyakumbuka maneno ya Dkt Salimin Amour ambaye aliwahi kuwa Rais wa Zanziba ambayo aliyatamka katika mkutano mmoja wa kisiasa.

“Hamjamboooo!, Wazimaaa!, Mupooooo!, Mupo tayariiiiii!, Asanteni Sana, Asanteni Sana na mimi nipo Tayari.” Maneno hayo aliyasema Dk Amour kuwa nayeye yu tayari katika mapambano ya kisiasa, japokuwa wakati huo alikuwa tayari yu mzee mno, akionesha kwamba kila mmoja wetu awe tayari pale anapohitajika. Niliwajibu kuwa na NA MIMI NIPO TAYARI.

Kikao kilipokuwa kinaendelea nilibaini ushiriki wa baadhi ya wajumbe ulivyokuwa mzuri iwe wale wa Zanzibar au wale wa Bara.Nilibaini kuwa baadhi ya taasisi nyingi za bara wengi wao wakuu wa baadhi ya taasisi walituma wawakilishi huku Zanzibar Wajumbe wake wakishiriki wakuu wenyewe wa taasisi hizo.

Hoja za ushirikiano katika matangazo baina ya Zanzibar na Bara ilijadiliwa kwa kina na pia hoja ya kutolewa kwa matangazo ya masuala ya kiserikali baina ya taasisi za umma nayo iliwekwa mezani.

“Tunashirikiana na TBC katika mambo kadhaa, iwe katika kurusha baadhi ya matangazo na hata baadhi ya matukio ya kitaifa kwa pamoja, ninatoa ahadi kuwa ushirikiano huo upo na tunajitahidi tutaboresha kama mjadala wa kikao hicho unavyoshauri.”

Alisema Dkt Salehe Mneno katika mojawapo ya azimio la kikao ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa ZBC. Kikao kilikwisha na kila mmoja kurejea kwake.

Baada ya juma moja, nilipewa jukumu la kuwasiliana na vyombo vya habari kadhaa nchini juu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na niliwaomba vyombo hivyo kunipatia Ankarakifani.

Niliwapigia simu ZBC kwa nambari iliyopokelewa na Dkt Mneno mwenyewe, nilimsalimu na kumueleza juu ya maombi yangu ya Ankarakifani, Mkurugenzi wa ZBC mwenyewe aliomba barua pepe yangu, nilipompatia tu baada ya dakika mbili nilipata Ankarakifano yao. Pia hali hiyo niliiona kwa Azam.

Huku taasisi zingine zikikichukua siku hadi mbili kupata hiyo nyaraka ya malipo, nilijifunza uhodari wa ZBC chini ya Dkt Mnemo katika kuitafuta pesa ya taasisi yake.

Kwa hakika binafsi sina nasaba na Dkt Mnemo lakini najaribu kueleza utendaji wake wa kazi kwa namna nilivyoweza kumuona kwa macho yangu mwenyewe.

Hoja yangu ya leo ni kuwa, Dkt Mnemo kuondolewa ZBC yaweza kuwa ni maamuzi sahihi au yakawa sivyo.Tabia ya mtu anayoifanya kwa mtu ambaye hamfahamu huwa inaweza kutoa taswira halisi ya mtu huyo kwa wengine na kwa nafasi yake. Naweka kalamu yangu chini nikiendelea kuomba sana Dkt Salehe Yussuf Mnemo apatiwe tahafifu ili aendelee kutoa mchango wake kwa Zanzibar na Tanzania yetu na watu kama hawa tunapaswa kuwalinda kwa gharama kubwa.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...