NA FARIDA SAIDY,
KILWA.
Wananchi wilayani
Kilwa mkoani Lindi, wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya
utalii kufuatia uamuzi wa dhati uliyochukuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), kufungua milango kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana katika
wilaya hiyo.
Wito huo umetolewa
hivi karibuni na Mkuu wa wilaya hiyo Bi. Zainabu Kawawa, ambapo amesema TAWA
inafanya kazi kubwa ya kutangaza utalii wa kusini hususan unaopatikana katika
wilaya ya Kilwa.
Ameongeza kuwa pamoja
na kazi kubwa inayofanywa na TAWA ya kutangaza vivutio vya utalii
vinavyowavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi. mamlaka hiyo imeweka
mazingira rafiki kwa watalii kwa kununua boti ya kisasa.
Mkuu huyo wa wilaya
amesema, boti hiyo ina uwezo wa kusafirisha watalii kutoka kisiwa kimoja hadi
kingine, huku wakifurahia kuangalia viumbe mbalimbali wa majini wakiwa ndani ya
boti hiyo.
Amesema utalii wa
majini unaopatikana katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, ni pamoja
na utalii wa Matumbawe, ambao watalii wanaweza kuona viumbe vya chini ya bahari
kupitia boti ya kisasa iliyonunuliwa na TAWA.
Vivutio vingine ni
utajiri mkubwa wa historia kupitia malikale (magofu), ambao kwa upekee wake,
umeingizwa katika orodha ya urithi wa dunia, inayotambuliwa kimataifa na
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO).
"Mbali na magofu
yanayopatikana, pia mtalii anapopata fursa ya kutembelea visiwa hivyo atapata muda
wa kufahamu historia nzima ya mji wa Kilwa na uzuri wake, tangu karne ya 13
pamoja na kufurahia upepo wa Pwani kutoka bahari ya Hindi," amesema.
Kwa upande wake Samson
Gisiri, Mhifadhi kutoka TAWA, ambao wamepewa dhamana ya kusimamia malikale,
alisema moja kati ya kazi ya mamlaka hiyo ni kusimamia na kutunza malikale
zilizopo katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Aidha, ameongeza kuwa
katika kuweka mazingira rafiki kwa watalii, TAWA imeanza kujenga sehemu maalumu
za malazi kwa ajili ya watalii Kilwa Kisiwani, ili kuwafanya wafurahie muda wao
katika visiwa hivyo.
Mhifadhi huyo
amewataka Watanzania kutembelea maeneo ya Songo Mnara na Kilwa Kisiwani, ili
kujionea urithi wa dunia unaopatikana katika visiwa hivyo.
Muongoza watalii abdalah akionesha moja ya magofu ya kale
yanayopatikana katika kisiwa cha Songomnara wilaya Kilwa mkoani Lindi, ambayo
yanayosimamiwa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania TAWA.

Muonekano wa viombe vya baharini ikiwa ni
moja ya kivutio kinachopatikana katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songomnara
wilaya Kilwa mkoani Lindi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...