Na. Veronica Mwafisi-Sumbawanga

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Sumbawanga, Bw. James Mbungano kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na mchakato wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, baada ya kushuhudia msingi wa jengo hilo la ghorofa ukifukuliwa ili kujengwa upya kwa viwango vinavyotakiwa.

Mhe. Ndejembi amesema, kitendo cha msingi wa jengo la ofisi hizo kufukuliwa kwa ajili ya kujengwa upya maana yake ni kuwa, kuna changamoto katika mchakato mzima wa kandarasi hiyo.

“Tumemsikia wenyewe Mhandisi akisema kuwa kulikuwa na changamoto ya mawasiliano kabla ya kuanza kwa ujenzi, hii ina maanisha kwamba kuna tatizo hapa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Ameongeza kuwa, kunapokuwa na makosa ya kimawasiliano ni ishara ya kukosekana utawala bora hivyo, Serikali inachokiangalia ni thamani ya fedha inayotolewa katika ujenzi kama inalingana na kiwango cha ujenzi.

Mhe. Ndejembi amemuhoji Mkandarasi anayesimamia ujenzi huo, Bw. Yohane Renatus kuhusu sababu ya ujenzi wa jengo hilo kutokamilika kwa wakati, na kuelekeza kasi ya ujenzi iongezwe bila kuathiri viwango stahiki.

Amesema haiwezekani fedha ya Serikali ikachezewa halafu Serikali ifumbie macho, hivyo itaendelea kuchukua hatua kwa watakaobainika ili thamani ya fedha iliyotumika ionekane kwa umma.

“Kama kuna watu wa kuwachukulia hatua tutawachukulia, huu ni uzembe, Mhe. Mkuu wa Wilaya tuanze uchunguzi wa mchakato mzima ili kubaini ulivyofanywa katika kumpata Mkandarasi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Deus Sanga amesema tangu wiki iliyopita ameweka kambi katika eneo hilo ambalo ujenzi wa Ofisi hiyo unaendelea ili kuhimiza ufanisi katika ujenzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...