Na Farida Said, Michuzi Blog

NAOMBA nikuazime muda wako japo kwa dakika chache tu nikuonjeshe kuhusu histori nzuri ya kupendeza na kuvutia ya eneo linaloitwa Kilwa Kisiwani.

Eneo hilo linalapatikana katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Kilwa Kisiwani ni moja ya eneo ambalo hapo zamani ilikuwa nchi inayojitegemea.Ndio ujue hivyoo!!

Kwa kutokea Makao Maku ya Wilaya ya Kilwa hadi kufika eneo la Kilwa Kisiwani ni takribani mwendo wa dakika takriban 15 hadi dakika 20 kwa kutumia usafiri wa boti inayokwenda kasi inayomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA).

Kabla ya kuendelea naomba nitumie nafasi hii mapema kabla sijawahi kutoa shukrani zangu za dhati kwa TAWA. Wao ndio walioniwezesha kufika Kilwa Kisiwani na baada ya kufika nimeona mengi na mengine ndio haya nawaeleza.Sina hiyana wala sina choyo tega sikio lako kwa umakini.

Nikiwa Kilwa Kisiwani nikakumbuka ule msemo wa Wahenga wetu na ile misemo yao ya kwamba 'Yakale Dhahabu'. Nikiwa katika eneo hilo hakika nimejiridhisha kweli Yakale Dhahabu'.

Ngoja nikwambie, ukifika katika Kisiwa hicho kabla ya yote utapokelewa na upepo mwanana wa Pwani ya Bahari ya Hindi.Upepo unaovuma na kuleta raha wala sio karaha,kweli kabisa nakwambia.

Ukifika katika Kisiwa hicho pia utashuhudia fukwe, malikale yakiwemo Magofu yaliyoachwa na Masultani waliopata kuishi katika Mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani vinachagiza mvuto wa eneo hilo la Pwani ya Mashariki ambalo lilikaliwa na jamii tofauti.

Iko hivi ukisoma historia ya Mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani utaona hapo zamani haukuwa mji bali ilikuwa nchi inayojitegemea, kwani ilikuwa na utawala wake pamoja Sarafu (Fedha yake). Kwa lugha rahisi kisiwa hicho kilikuwa kimetimia kwa kila kitu 

Katika eneo hilo kwa sasa yamebaki magofu na malikale na kufanya kuwa vivutio vya utalii, hasa utalii wa malikale. Katika kuhakikisha uhifadhi wa utalii huo unakuwa endelevu kizazi hadi kizazi TAWA wamepewa jukumu la kusimamia eneo hilo.

TAWA wamekuwa wasimamizi wa Kilwa Kisiwani tangu mwaka 2018/20019 na hakika eneo hilo limekuwa kivutio kikubwa, Hivyo, watalii kutoka ndani na nje yaTanzania wamekuwa wakifika eneo hilo, kwanza kuona vivutio vya utalii, pili kujifunza historia ya kisiwa hicho .Nikukumbushe kabla ya kuwa chini ya TAWA eneo hilo lilikuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Malikale 

Hata hivyo, uwepo wa majengo ya zamani na mabaki ya kiikolojia yanayopatikana Kilwa Kisiwani na Kisiwa cha Songo Mnara yanaelezea maendeleo ya kijamii, kibiashara na kiutamaduni ya watu wa Pwani ya Afrika Mashariki kati ya karne ya tisa na 19 baada ya Kristo 

Inaelezwa kwamba kushamiri kwa biashara mbalimbali ikwemo biashara ya shanga, pembe za ndovu na nyinginezo katika karne ya 11 na 16 katika Kisiwa hicho jamii tofauti zilizifika na kuishi hapo, baadhi ya jamii hizo ni Washirazi, Wareno, Waajemi, Wamalindi kutoka Kenya, Warabu wa Oman, Wajerumani pamoja na Waingereza.

Uhalisia, uhalali na historia yake ndivyo vinafanya mji huo kuwa na umuhimu na wa kipekee kwani kila jamii iliyoishi eneo hili iliacha aina fulani ya kumbukumbu.

Ukiwa katika Kisiwa hicho utaona Msikiti mkuu na mkongwe zaidi wa kisultan Pwani ya Afrika Mashariki uliokuwa ukitumiwa na masultani katika karne ya 9 ambao nao umekuwa kivutio kikubwa cha watalii.

Mhifadhi kutoka TAWA ambao wamepewa dhamana ya kusimamia malikale hizo, Samson Gisiri, anafafanua kwa kina jitihada zinazoendelea kufanywa katika kuhifadhi na kutunza urithi wa Kilwa ziliongezeka hasa kuanzia miaka ya 1900.

Anasema baadhi ya vioneshwa (vitu vya kale) vilivyohifadhiwa kwenye makumbusho hayo ya kihistoria ya mji mkongwe Kilwa Kisiwani ni pamoja na Ndatu (kandambili za asili).

"Kandambili hizo ni za watu wa Kilwa Kisiwani zilizotengenezwa na minyaa, zilikuwa zinatumika na wavuvi katika kipindi hicho cha kale. Pia, kuna vioneshwa vingine kama Dema (mtego wa Samaki).

"Mtego huo wa samaki wa asili unaotumiwa na wavuvi kwenye kina kirefu cha maji lakini pia kuna Nanga iliyotengenezwa kwa jiwe lenye urefu wa mita 1.2 na upana mita 0.35 na inasadikika ilitengenezwa India au nchi nyingine ya Uarabuni," amesema.

Gisiri anasema jitihada zinazofanywa na TAWA katika kutangaza malikale katika Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara zinaendelea kuleta tija kwani watalii wengi wanatembelea Visiwa hivyo.

Anaongeza Mamlaka hiyo imeanza kujenga sehemu maalumu ya mapokezi na malazi kwa ajili ya watalii wanaotembelea mji huo mkongwe wa Kilwa Kisiwani ili kuwafanya wafurahie muda wao ndani ya visiwa hivyo.

“Utalii wa majini ni kivituo kikubwa cha watalii hapa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, watalii wanaweza kuona chini ya bahari matumbawe na viumbe vingine kupitia boti ya kisasa iliyonunuliwa na TAWA,"anasema Gisiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Zainabu Kawawa anasema watalii zaidi ya 120 kutoka mataifa mbalimbali duniani yakiwemo ya Marekani, Japan, Uingereza, Ujerumani na Uswisi walifika katika eneo hilo Desemba 2021 na meli ya kisasa ya Le Bellot.

"Hii ni ishara nzuri ya kuifungua Kilwa kiuchumi. Uamuzi uliochukuliwa na TAWA wa kufungua milango kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana wilayani Kilwa hasa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ni sehemu ya fursa kwa wananchi kuanza kuwekeza kwenye sekta ya utalii.

“Hii ni fursa iliyojitokeza wilayani kwetu ni vyema wananchi sasa wajitokeze kuwekeza kwenye ardhi zao kujenga hoteli za kitalii, nyumba za kisasa za kulala wageni ili kukidhi mahitaji ya watalii siku za usoni,” anasema Zainabu.

 

Moja ya jengo la Msikiti wa kale ulikuwa ukitumiwa na Masultani katika Kisiwa cha Kilwa Kiiwani.

. Gofu la kale lilkuwa likitumiwa na Wareno kama Gereza ambapo kwa sasa limekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaofika katika Kilwa Kisiwani.

Muongoza watalii Bwana. Abdalah  Ahmad akionyesha vitu vya kale vilivyohifadhiwa kwenye makumbusho hayo ya kihistoria ya mji mkongwe Kilwa Kisiwani ni pamoja na Ndatu (kandambili za asili) na zana za uvuvi ziliaokuwa zikitumika na watu wa kale.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...