Na Seif Mangwangi, Arusha

UKOSEFU wa maadili umeelezwa kuendelea kukua kwa kasi miongoni mwa baadhi ya vijana mkoani Arusha ambapo hivi sasa wameanza kuwaita wazee wao majina ya kejeli kama 'Malboro', mfuko wa nailoni uliopigwa marufuku kuuzwa nchini.

Wakizungumza katika misa maalum ya kuwalisha wazee na kuwakumbuka kwa mambo mema ambayo waliyafanya wakati wa ujana wao katika kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria Unga Ltd, wazee hao walisema vijana wa hivi sasa wamekuwa wakichanganyikiwa kutokana na kukosa baraka za wazee wao.

"Sisi wazee tunaitwa Malboro, ule mfuko ambao Hayati Dkt Magufuli aliuzika, vijana wetu wakitaka kuoa mwanamke anaanza kumuuliza mpenzi wake Malboro zipo? akimaanisha kama sisi wazee ambao ni wazazi wa mwanaume bado tupo hai na kama tupo basi huyo mwanamke atahakikisha anatusambaratisha,"amesema mzee Raymond Msemo.

Hata hivyo amesema kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikiwadanganya kuwalipa wazee mafao ya kila mwezi kwa kuwa hawawezi tena kuendelea kufanyakazi na hivyo kuikumbusha kutimiza ahadi hiyo ili waweze kuishi maisha ya amani na kuepuka manyanyaso kutoka kwa vijana wao kwa kuwa watakuwa na kipato cha uhakika.

Amesema kukosekana kwa mafao kumekuwa kukisababisha kuishi maisha duni na kupelekea kudharauliwa na vijana waliowazaa wenyewe kwa kuwa wamekuwa tegemezi.

" Tunawasihi vijana wabadilike, watuheshimu wazee, vijana siku hizi wanakula dawa za kulevya, waache warejee kanisani, sisi zamani hatukuwa hivyo na ndio sababu tumebarikiwa kuwa na umri mrefu zaidi," alisema mzee Msemo.

Kwa upande wake Paroko wa Kanisa hilo Padre Festus Mangwangi, amesema mmomonyoko wa maadili miongoni mwao vijana umekithiri sana katika miaka ya hivi karibuni na hivyo kuwaomba wazee kutumia busara zao kukemea vitendo hivyo.

Akizungumza wakati akiendesha Misa takatifu kanisani hapo Padre Mangwangi amesema vijana wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo viovu kama ulevi, ushoga, wizi, ubakaji na ulawiti jambo ambalo limekuwa likimkasirisha Mungu.

"Siku hizi majanga hayaishi kwa sababu kila siku vijana wanamkasirisha Mungu kwa kufanya vitendo viovu, nawaomba wazee wangu kushirikiana na kanisa tukemee hivi vitendo," amesema.

Padre Mangwangi amesema Kanisa hilo limekuwa na utaratibu wa kuhudumia wazee ikiwemo kukaa nao na kupata chakula mara mbili kwa mwaka na kwamba kupitia kanda 15 na jumuiya 74, kanisa limekuwa likihudumia zaidi ya wazee 300.

Amesema lengo la hafla hiyo ni kuwakumbusha watoto thamani ya wazee, kuwajali na kuwathamini.

" Wako watoto wenye nafasi na kazi nzuri lakini hawawataki wazee wao, tunafanya hili zoezi ili watoto wajue uthamani wazee wao, lakini pia ili waweze kutubariki tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri na ktk njia ipasayo," Amesema.

Ameongeza "tunapenda pia kuwaenzi wazee sababu wana nafasi kubwa ya kukemea maovu kwenye jamii, hasa watoto wao na wakisema watoto wanaweza kuacha," Amesema.

Kwa mujibu wa Padre Mangwangi,hafla hiyo ambayo inafanywa na kanisa hilo kipindi hiki pia imepata Ufadhilii kutoka katika familia ya Fabiene Jaquemet raia wa Uswis ambaye yuko nchini kama volunteer ambapo mbali ya wazee kupata chakula pia walipewa Sh.10,000 kila mmoja.
Paroko wa parokia ya Moyo safi Padre Festus Mangwangi akiwagawia fedha wazee mara baada ya kuwafanyia misa ya kuwaombea na kula nao chakula cha pamoja.

Volunteer Fabiene Jaquemet Raia wa Uswis akigawia fedha wazee

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...