Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Ally Possi, ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kubuni vyanzo vya mapato ambavyo ni himiilivu na visivyoumiza washitiri ili kuisaidia taasisi kujiendesha na kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Possi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Mamlaka hiyo na kusema kuwa ongezeko la mapato litapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya watumishi kuhama kwani mapato yataweka mazingira mazuri kwa watumishi.
“Nikupongeze sana Mkurugenzi Mkuu kwani kazi yako inaonekana sababu utabiri kwa sasa ni wa kuaminika kwa asilimia zaidi ya 80 lakini fikirieni kuja na vyanzo vya mapato visivyoumiza washitiri wenu ili mtumie sehemu ya mapato hayo kama motisha kwa watumishi wenu", amesisitiza Dkt. Possi.
Dkt. Possi amesema kuwa Serikali iko tayari kushughulikia changamoto zote zinazoikabili Mamlaka hiyo ikiwemo changamoto za kuhama kwa watumishi ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa imara.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa ili kuongeza uhakika wa taarifa kwa kuwa sekta ya hali ya hewa inazitegemeza sana sekta nyingine hususani za usafirishaji pamoja na kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa Mamlaka imejipanga kikamilifu kuboresha miundombinu pamoja na kusomesha watumishi ili kuendeleza weledi katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi yuko katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam ya kutembelea taasisi zilizo chini ya sekta hiyo ili kuona shughuli mbalimbali za kiutendaji na kujadili namna bora ya kupata suluhu ya chagamoto zinazowakabili.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi, kuhusu utendaji wa Mamlaka hiyo wakati Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa na Utafiti wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a, wakati alipotembelea ofisi ya uchakataji taarifa za hali za hali hewa, jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akisisitiza jambo kwa viongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi na Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hew ana Utafiti wa Mamlaka hiyo, Dkt. Ladislaus Chang’a.
Sehemu ya Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dky Ally Possi (hayupo pichani) wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akimwonesha Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, DKt. Ally Possi, namna ya utabiri unavyofanyika, wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa na Utafiti wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, kuhusu shughuli za utabiri wakati Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea ofisi za Mamlaka jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...