Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo amemshukuru Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania chini ya Mkurugenzi Suzan Bipa kwa kutambua thamani ya mtoto wa kike kwa kumuwezesha kupata elimu ya TEHAMA kwa kuanzisha mradi wa Skills For Their Future kwa Shule tatu za Sekondari za Karibuni, Wailes na Miburani
Jokate Mwegelo amewataka walimu wa Shule za Sekondari Karibuni, Wailes na Miburani kuzitumia kwa uweledi kompyuta 120 watazokabidhiwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania kwa ajili ya kumuandaa mtoto wa kike wa baadae
Amesema, amesema taasisi ya BRAC imekuwa na mchango mkubwa wa elimu kwa shule za msingi na Sekondari ambapo kwa mara ya kwanza walianza mwaka 2020 na kufanikiwa na kwa sasa mradi huu utawafikia wanafunzi 600 kutoka katika shule hizo.
Jokate amesisitiza Wadau wa elimu waendelee kutoa michango yao kupitia sekta ya elimu kwa kushirikiana na Serikali ili kuzidi kuboresha elimu na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha mtoto anapata elimu bora.
“Kiukweli taasisi ya BRAC Tanzania kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Suzan Bipa imekuwa na mchango mkubwa kayika sekta ya elimu, Naomba walimu na wanafunzi Kompyuta hizi 120 zilizokabidhiwa kwenu mkazitumie kwa ajili ya kujijenga kiakili, kiuwezo kupitia TEHAMA ili muwe moja ya wataalamu wakubwa wa teknolojia nchini,”amesema Jokate
Akizungumzia mradi huo Mkurugenzi wa shirika la BRAC Maendeleo Tanzania Susan Bipa amesema kuwa “Tafiti zinaonyesha kuwa ni wanawake na wasichana wachache nchini Tanzania ambao wanashiriki katika fani ya TEHAMA na kadiri ya asilimia 25 tu ya wanawake wanaofanya kazi za teknolojia nchini Tanzania.
Amesema “Hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya kutosha na pia ujuzi mdogo wa walimu kuweza kutoa mafunzo husika kwa wanafunzi. Na hivyo basi kupitia mradi huu tunategemea kuzikabili changamoto hizi kwa kuweka miundombinu husika, vifaa vya ufundishaji ikiwemo kuongeza uwezo kwa walimu.”
Bipa amesema, Lengo kuu la mradi huu unalenga kushughulikia changamoto zinazozuia wasichana na wanawake wadogo (Adolescent Girls and Young Women - AGYWs) kuweza kupata huduma za TEHAMA na kuzitumia kwa ufanisi ili kuboresha ujuzi katika ujasiriamali na kuongeza uwezo wa kuajiri.
Ameongeza kuwa, Kupitia mradi huu inategemewa kuwa ushiriki wa wasichana katika TEHAMA utaongezeka ili kuongeza fursa zaidi za ajira kwa wasichana katika sekta ya teknolojia. Mradi utanufaisha wasichana 600 kutoka Shule za Sekondari za Karibuni, Miburani na Wailes zilizopo wilaya ya Temeke – Dar es Salaam. Vilevile mradi utaboresha uwezo wa walimu 45 kutoa mafunzo bora ya kusoma na kuandika kwa njia ya kidijitali katika shule hizo.
Kila shule inayoshiriki katika mradi huo itakabidhiwa kompyuta 20 aina ya laptop, na tablets 20 kwa kufundishia na kufanyia mazoezi, hali kadhalika shirika limekarabati darasa moja kwa kila shule ambalo litatumika kama maabara za kompyuta (computer labs).
Skills for their Future ni mradi ambao BRAC Maendeleo uliutambulisha mwaka 2020 kama majaribio katika shule ya Sekondari ya Temeke ambapo wasichana 30 wanaochukua mchepuo wa Sayansi walinufaika wakiwemo walimu 18 wa shule hiyo. Mradi huu unafanyika chini ya ufadhili wa shirika la TheirWorld lenye makao makuu nchini Uingereza.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akizundua chumba cha Kompyuta kitakachotumika kwa ajili ya kujifunzia masuala ya TEHAMA kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Karibuni ikiwa ni mradi wa Skills For their Future unaoratibiwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania kwa Shule za Karibuni, Wailes na Miburani zote za Wilaya ya Temeke
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...