Huawei, TTCL Zasaini Makubaliano Kuboresha Teknolojia Ya Mawasiliano
Kampuni ya Mawasiliano ya TTCL na Kampuni ya Teknolojia ya Huawei, wametia saini hati ya Makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji utakaoziwezesha pande hizo kushirikiana katika kuboresha teknolojia ya mawasiliano nchini ikiwemo uunganishaji wa huduma ya uhakika ya mtandao wa intaneti majumbani (FTTH),upanuzi wa huduma wa huduma ya internet yenye kasi (4G), na upanuzi wa huduma hizo hususani maeneo ya vijijini.
Hati iyo ya ushirikiano ilisainiwa katika kilele cha siku ya Biashara kwa Tanzania katika maonyesho ya Biashara ya Dubai Expo 2020 yaliyofanyika, Dubai, Falme za Kiarabu hivi karibuni ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumzia Makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw.Waziri Kindamba alisema ushirikiano huo alieleza kuwa Makubaliano hayo yanalenga katika kuziwesha pande zote mbili kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kiutendaji hatua ambayo italisaidia shirika hilo kujijengea uwezo wa kiufanisi hususani katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapitia mabadiliko ya kidijitali yanayoakisiwa na ongezeko la watu wanaounganishwa kwenye huduma za mawasiliano na mtandao.
“Naweza kusema ushirikiano huu na kampuni ya Huawei Technologies umekuja wakati mwafaka sana, kwani kwa kiasi kikubwa utachangia katika kuifanya nchi yetu kuwa ya kidijitali. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila mteja anaunganishwa na huduma za mtandao za haraka na bora.’’ Alisema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Huawei Tanzania, Bw. Damon Zhang alisema kuwa nia ya Kampuni ya Huawei katika kushirikiana na TTCL ni matokeo ya kutambua kuwa miundombinu ni jambo lenye umuhimu zaidi katika maendeleo ya sekta yoyote, hasa sekta ya Mawasiliano.
“Hatua yetu ya kushirikiana na TTCL ni matokeo ya Huawei kutambua ukweli kwamba miundombinu ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini. Tunawahakikishia dhamira yetu ya kuendelea kushirikiana na serikali na mashirika yake ili kuhakikisha Tanzania inaunganishwa kikamilifu’’. alisema
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara pamoja na kupongeza hatua hiyo, alisema kuwa ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili utaijengea uwezo kampuni ya Mawasiliano ya TTCL katika sekta ya TEHAMA na maeneo mengine.
Utiaji saini wa hati ya Makubaliano kati ya Kampuni ya Teknolojia ya Huawei na TTCL ulishuhudiwa pia na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano ya TTCL Bw Waziri Kindamba (Kulia walioketi) na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Teknolojia ya Huawei Tanzania, Bw. Damon Zhang (Kushoto walioketi) wakitia saini hati ya Makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji utakaoziwezesha pande hizo mbili kushirikiana katika kuboresha teknolojia ya mawasiliano nchini. Makubaliano hayo yalisainiwa katika kilele cha Siku ya Kitaifa ya Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Dubai Expo 2020 yaliyofanyika Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu UAE hivi karibuni ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi. Anaeshuhudia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (Nyuma)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...