Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Jerry Muro akizungumza na Wananchi na Wana CCM wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo katika hafla ya Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanyika jana Viwanja vya Hospitali hiyo  ambayo ujenzi wake unaelekea kukamilika hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa akihutubia katika hafla hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika hafla hiyo Leon Katanga akizungumza kwenye hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye hafla hiyo. Wengine katika picha ni Madiwani.Chifu Mkuu wa Kabila la Wanyaturu Wilaya ya Ikungi, Mjengi Gwao akizungumza kwenye hafla hiyo.Muonekano wa baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Ikungi ambayo yalikaguliwa na Wananchi wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Wananchi wakiendelea na ukaguzi wa majengo ya hospitali hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikugi Jerry Muro akisalimiana na Katibu wa CCM wa wilaya hiyo Stamili Dendegu wakati wa ukaguzi wa majenge ya hospitali hiyo.

Mdau Charles Akio akiwa kwenye hafla hiyo.Hafla ikiendelea.
Hafla ikiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu.Hafla ikiendelea. Kutoka kushoto ni ,Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Ally Rehani, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Abubakar Muna na Mchungaji wa Kanisa la Wasabato (SDA) Wilaya ya Ikungi, Joseph Metarus.

Hafla ikiendelea.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakiwa kwenye hafla hiyo. Kushoto ni Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Ihanja Mariam Ntembo.
Waandishi wa habari wakichukua matukio kwenye hafla hiyo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi Stamili Dendegu akizungumza kwenye hafla hiyo wakati akimkalibisha mgeni rasmi Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Mika Likapakapa. (hayupo pichani)

Mohammed Omari (kulia) akila kiapo baada ya kujiunga na CCM akitoa Chadema. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa CCM Kata ya Ikungi, Stamili Dendegu na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa.
Burudani zikirindima kwenye hafla hiyo.
Wana CCM wakiserebuka wakati wa sherehe hiyo.


Na Dotto Mwaibale, Singida.


MACHI 19, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan ametimiza mwaka mmoja tangu ale kiapo na kushika wadhifa wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya tano Hayati  John Pombe Magufuli. Katika kipindi hiki Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali ya awamu ya sita anayoiongoza ameendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025 kwa kasi kubwa. 

Mafanikio ya utekelezaji huo wa Ilani  ni mengi na hapa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Jerry Muro anayataja baadhi wakati akihutubia katika hafla ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanyika jana Viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Ikungi  ambayo ujenzi wake unaelekea ukingoni akianza na  sekta ya ulinzi.

 

                                        ULINZI NA USALAMA WA TAIFA                                    

Muro anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 - 2025 Ibara 105 katika miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuhimiza Serikali zake kuimarisha Ulinzi na Usalama wa nchi yetu, raia wake na mali zao ili kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu ambazo ni tunu kuu za Taifa letu.  

Anasema uhakika wa amani, ulinzi na usalama ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kuishi na kuendelea na shughuli zao za maendeleo. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan wilayani Ikungi imeendelea kuhakikisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatekeleza majukumu yake katika mazingira yaliyoboreshwa hivyo kuhakikisha Wilaya ya Ikungi na Mkoa mzima wa Singida unakuwa salama na Wananchi wake wanatekeleza majukumu yao katika hali ya usalama, umoja, mshikamano na utulivu. 

                                                                        MUUNGANO                                                                       


Akizungumzia Muungano Muro anasema katika kipindi cha mwaka mmoja  Rais ameendeleza na Kudumisha Muungano wa Tanzania ambapo kero 11 za Muungano zimetatulika. 

                                     DIPLOMASIA YA SIASA NA UCHUMI                             


Muro akizungumzia Diplomasia anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025 Ibara 132 (a) katika Diplomasia Siasa Chama kinaelekeza Serikali kuboresha utekelezaji wa mipango ya kuimarisha Diplomasia ya Siasa ya kimkakati kwa ajili ya kulinda Amani, Uhuru, Masilahi ya Taifa na kuimarisha ujirani mwema. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi wameendelea kunufaika na jitihada za Serikali kukuza mahusiano ya kiuchumi na Mataifa, Jumuiya za Kikanda na Taasisi za kimataifa ambapo Wilaya ya Ikungi wamefaidika na miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na Taasisi ya KOICA pamoja na UN WOMEN kwa kuwawezesha baadhi ya Mabinti  kutoka Wilaya ya Ikungi kupelekwa masomoni, baadhi ya Vikundi vya Wananchi kuanzisha Miradi ya Mbogamboga kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa katika Vijiji vya Kipumbwiko na Mnang’ana, kujenga Ghala la Alizeti katika Kijiji cha Mnang’ana, kupima na kutoa Hati Mililki za Kimila 6100 ambapo Hati 5050 zimeshagawiwa kwa Wananchi mbalimbali ambapo kati yake Hati 2030 zimegawiwa kwa Wanawake.  Miradi yote hii imegharimu kiasi cha Sh. Bilioni 5. 

Anasema  Rais amefanya ziara mbalimbali katika Nchi tofauti tofauti kwa lengo la kukuza Diplomasia ya Siasa na Uchumi wenye lengo la kutunufaisha Wana Ikungi na Watanzania wote kwa ujumla.

Muro anasema   Aprili 11,  2021 Rais alifanya ziara yake ya kwanza nje ya Tanzania na ziara hiyo ikiwa na lengo la kusaini makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta. Ujenzi wa bomba hili unapita katika Mkoa wa Singida katika Wilaya za Iramba, Mkalama na Singida, Bomba hili kupita jirani na Wilaya yetu kunatengeneza ajira kubwa kwa watu wetu, utaongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na ni chanzo kingine cha uchumi wa Taifa letu baada ya Mradi huu kukamilika. 

Anasema  Mei 4 , 2021 Rais alifanya ziara nchi ya Jamhuri ya  Kenya pamoja na mambo mengine akahutubia wananchi wa Kenya. 

“ Ni ziara yenye tija kwa uchumi wa Nchi ambayo imeleta matokeo makubwa na zaidi ya vikwazo 46 kati 64 vya kibiashara baina yetu na nchi ya Kenya vimeondoka” anasema Muro. 

Muro anaendelea kusema Novemba 10, 2022 Rais alifanya ziara ya siku tatu nchini Misri ambapo ulishuhudia utiwaji saini ya Nyaja za Uwekezaji baina ya nchi yetu na Misri baada ya ziara ile Nchi yetu imeendelea kupokea Wakezaji wengi kutoka Misri ambao watawekeza bilioni 460 katika ujenzi wa viwanda ambapo na  Wananchi wa Ikungi wamejiandaa kuwapokea baadhi ya Wawekezaji watakaofika wilayani humo.

Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro anasema Septemba 23, 2021,. Rais alifanya ziara Marekani na kuhutubia kwa mara ya kwanza mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo  alilipatia Taifa letu heshima kubwa. 

Anasema Februari 10, 2022  Rais alifanya Ziara Ufarasa na Ubeligiji pamoja na mambo mengine Ziara hiyo ilifanikisha kusainiwa kwa mikataba 6 na kiasi cha Euro milioni 178 mkopo wa masharti nafuu umepatikana kwa ajili ya kughalamia mradi wa ujenzi wa barabara wa mabasi yaendayo haraka. Pia kiasi cha Euro 80 kimepatikana ili kuimarisha Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania ambayo tunaamini  itanufaisha Wananchi wa Wilaya ya Ikungi. 

Anasema Februari 25, 2022  Rais alifanya Ziara UAE- Dubai wakati wa mkutano wa Biashara na Uwekezaji Rais alishuhudia kutiwa saini kwa Hati (MoU) 36 za Kimaendeleo ambapo idadi ya Ajira zinazotarajiwa kupatikana kwa ujumla kutokana na makubaliano hayo ni zaidi ya Ajira 200,000 katika kipindi cha miaka 4 huku uwekezaji huo ukigharimu zaidi ya trilioni 17.35 za Tanzania. 

“Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kufungua nchi kiuchumi na kuimarisha Diplomasia” anasema Muro. 

                                                                    KILIMO                                                            


Akizungumzia kuhusu sekta ya kilimo Muro anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 - 2025 Ibara ya 37, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kusimamia mapinduzi ya kilimo ili kuhakikisha kinaendelea kuwa chenye tija na kinachotumia teknolojia ya kisasa. 

Aidha, chama kitahakikisha kuwa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) inaendelea kutekelezwa na kutoa mchango mkubwa katika usalama wa chakula, pato la Taifa, maendeleo ya sekta ya viwanda. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Wilaya ya Ikungi kuendeleza mashamba ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ya Mikorosho na Miparachichi katika Vijiji vya Mkiwa na Ulyampiti, ambapo katika kipindi hicho Halmashauri ya wilaya hiyo  imepokea Sh. 4,500,000 kwa ajili ya kuendeleza mashamba hayo na Mradi huu bado unaendelea.

                                                                            ELIMU                                                                        


Muro anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/2025 Ibara ya 80 imesema Chama Cha Mapinduzi kinatambua umuhimu Sekta ya Elimu na mchango wake katika ajenda ya maendeleo kwa kuandaa mtaji watu wenye uwezo wa kutumia fursa za rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo na kuchangia katika jitihada za nchi kufikia uchumi wa kati uliojikita katika misingi ya viwanda. 

Anasema chama katika miaka mitano ijayo, kinalenga kuimarisha ubora wa elimu katika ngazi zote kwa kuzingatia falsafa ya kujitegemea yenye kuendana na mazingira ya nchi yetu, hususan elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi VETA.

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi wamefanikiwa kupata fedha zaidi za ukamilisha wa Chuo cha Ufundi VETA ambacho tunatarajia kitakamilika mwanzoni mwa mwezi Mei 2022.  

Aidha, wamefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa 79, vyoo na miundombinu ya maji 18 katika shule za msingi mbalimbali ambapo pia wamepokea jumla ya Sh. 628,002,811 kama fedha za Mpango wa Elimu Bila Malipo.  

Anasema katika Elimu ya Sekondari  wamepokea jumla ya Sh. 940,000,000 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa Shule za Sekondari Matongo na Makilawa. Wamepokea kiasi cha Sh. 1,340,000,000   kwa ajili ya ujenzi wa vyumba madarasa 67 katika shule za Sekondari.

“Tumepokea Sh. 81,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Utawala katika shule ya Sekondari ya Issuna na ujenzi wa miundombinu ya maji katika shule ya Sekondari Dadu. Tumepokea  Sh. 100,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Sekondari Dr. Shein, ukamilishaji wa madarasa Shule ya Sekondari Lighwa, Ukamilishaji wa madarasa katika shule ya Sekondari Ntuntu, Ukamilishaji wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Sepuka na Ukamilishaji wa madarasa katika Shule ya Sekondari Utaho” anasema Muro.  

Aidha Muro anasema jumla ya Sh. 367,851,448  zimepokelewa kama fedha za mpango wa Elimu Bila Malipo.  Miradi hiyoi imewazesha kuwa na miundo mbinu mizuri ya Elimu kwa watoto hali iliyoongeza moyo wa kupenda shule kwa wanafunzi wanaoitumiai.

  AFYA                                                            

Muro anasema kuwa katika Ilani ya CCM 2020/2025 Ibara ya 83 imeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutoa kipaumbele katika Sekta ya Afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa Taifa letu. Lengo la Chama ni kuhakikisha Wananchi wanakuwa na afya na siha bora ili kuwawezesha kushiriki katika shughulli za ujenzi wa Taifa na kuboresha maisha yao. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 2.8 ambazo zimetumika katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Sekta ya Afya katika wilaya hiyo ambapo ujenzi wa Zahanati za Kinyampembee, Makotea, Misule, Mlandala, Mnang’ana, Mpugizi na Issuna unaendelea kufanyika.

Anasema ujenzi mwingine unaoendelea ni  wa Vituo vya Afya vya Irisya, Iglansoni, Ntuntu na Iyumbu,Ukamilishaji wa Hospitali ya Wilaya, Ujenzi wa Nyumba ya Watumishi katika Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa vyoo vya zahanati za Dung’unyi, Nkuwi, Matongo na Matyuku. 

                                                                            MAJI                                                                            


DC Muro anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020- 2025 ibala 100. katika miaka mitano ijayo, lengo la CCM ni kuona kuwa nchi inaendelea kuwa na usalama wa maji na kwamba huduma ya majisafi na salama inaendelea kuimarishwa na kuwafikia zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo mwaka 2025. Aidha, CCM inalenga kuhakikisha kuwa Kaya nyingi zaidi mijini zinaunganishwa katika mtandao wa maji taka. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Machi 2022 Serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya Sh. Bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi ya miundombinu ya maji katika Vijiji vya Lighwa, Mtunduru, Ulyampiti, Ikungi, Matare, Ihanja, Irisya, Iglansoni na Igombwe. 

Anasema Miradi inayoendelea ikikamilika itaongeza asilimia ya upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 55 ya sasa hadi kufikia asilimia 65 ambayo ni sawa na wazi 219,640 kati ya Wakazi 337,907.

UJENZI NA UCHUKUZI                

Muro anasema katika Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 -2025 Ibara ya 55 inasema katika miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaelekeza Serikali kuendeleza shughuli za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuifanya Sekta ya Ujenzi ifikie malengo yake ya kuwezesha wananchi kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato chao. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan  Wilaya ya Ikungi wamepokea Nyongeza ya Bilioni 2  kwa ajili ya kufungua maeneo ambayo hayapitiki (hayana barabara) vijijini ambapo hadi sasa wameshapokea kiasi cha Sh. 828,361,074.14 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Utaho – Makiungu na Siuyu – Nali – Makotea yenye jumla ya Km 17.84, Mungaa – Ntuntu – Mang’onyi na Issuna – Ngongosoro – Ilolo yenye jumla ya Km 22.52.  Barabara ya Igombwe – Makhonda – Mwaru yenye jumla ya Km 13.2 na ujenzi wa daraja la Mto Ngano katika barabara ya Mtamaa – Minyughe – Mtavile yenye jumla ya Km 4 na barabara ya Sepuka – Italala yenye urefu wa Km 2.75. 

Aidha Muro anasema wameidhinishiwa kiasi cha Sh. Bilioni 1 kwa ajili ya Matengenezo ya barabara katika wilaya hiyo  ikiwa ni miradi ya barabara kwa kila Jimbo Sh. milioni 500 ambapo mpaka sasa zimekwishapokelewa Sh. milioni 900 kwa ajili ya miradi hiyo ambapo wanatarajia zitumike kutekeleza barabara ya Misughaa – Msule – Sambaru yenye urefu wa Km 15.5 pamoja na ujenzi wa karavati sanduku 6 na kalavati misitari 13 pamoja na barabara za Mtunduru – Sepuka na Irisya – Unyinga zenye urefu wa Km. 24.3 kalavati sanduku 1, Kalavati misitari 11 na kivuko (driff) 1. 

UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO 


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro anasema katika ilani ya uchaguzi ya CCM ibara 239, 241 na 243 Chama kina lengo la kuchochea na kuhamasisha na kuendeleza jamii Utanzania, kuburudisha, na kuongeza fursa za ajira kupitia Utamaduni, Sanaa na Michezo. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan katika wilaya hiyo wameweza kushirikiana na Wadau mbalimbali kuhamasisha shughuli za Utamaduni Sanaa na Michezo ambapo wamefanikiwa kuanzisha mashindano mbalimbali ya michezo ya Mpira wa Miguu kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Majibo ya Singida Mashariki na Magharibi. Aidha, katika kudumisha mila na tamaduni zetu wamewawezesha na kushiriki usimikwaji wa Watemi katika Tarafa za Ihanja, Ikungi na Mungaa. Aidha, Vikundi mbalimbali vya Sanaa za Maonyesho wamewezeshwa kupitia vikundi vyao kuweza kufikia malengo waliyojipangia. 


  VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI                

Anasema katika ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 ibala ya 46 na 49 Kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Viwanda na Biashara, Chama Cha Mapinduzi kitaelekeza Serikali kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kubuni mikakati zaidi ili kujenga uchumi wa viwanda jumuishi. 

Muro anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi wameweza kuwaalika na kuwawezesha Wawekezaji mbalimbali waliofika wilaya humo kwa nia ya kuwekeza katika Kilimo, Viwanda na Uchimbaji madini akitolea mfano wamefungua shamba la Alizeti lenye ukubwa wa Hekari 4500 na kuwaalika Wawelezaji tofauti tofauti kutoka ndani ya wilaya na nje  ili waweze kuwekeza katika kilimo cha Alizeti katika mashamba hayo, mwitikio ulikuwa chanya na umewashawishi kuufanya  mpango huo kuwa endelevu kwa lengo la kuifungua Ikungi kiuchumi.  Aidha, wamewezesha Kampuni ya Shanta Gold Mining kuendelea na Mradi wake wa uchimbaji dhahabu katika Kijiji cha Mang’onyi ambao una uwekezaji wa zaidi za Dola za Kimarekani Milioni 40, Uongozi wa Shanta umewahakikishia kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka huu. 

 Aidha Muro anasema watumetengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyabishara wadogo na wa kati kuweza kupata mazingira bora pamoja na vibali (Leseni) za kufungua na kufanyia biashara katika Wilaya ya Ikungi.


SEKTA YA HABARI                                


Muro anasema katika ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 ibala ya 125, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha Sekta ya Habari inaboreshwa ili kuwaongezea wananchi fursa ya kupata habari kwa kuongeza wigo wa upashanaji wa habari. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi wamekuwa na uwanda mpana wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni. Aidha, kumekuwepo na ushirikiano kati ya Viongozi wa Serikali na Waandishi wa Habari hali inayopelekea wilaya hiyo kusikika na kufahamika zaidi kupitia vyombo vya Habari.

 

SEKTA MALIASILI                          

                         

Anasema katika ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 ibara ya 69, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuimalisha usimamizi, ulinzi na uhifadhi Maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho. 

Muro anasema kuwa katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi imeanzisha mchakato wa kuhifadhi msitu wa Minyughe kwa kuanzisha mchakato wa kuhamisha umiliki wa hifadhi ya Minyughe kutoka Halmashauri ya Wilaya na kuhamia Wakala wa Hudumu za Misitu Tanzania (TFS) ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh.65,512,599 zimetolewa na Serikali kwa lengo la ukaguzi, upimaji na uelimishaji.  Aidha, Wilaya imeendelea kusimamia Maliasili nyingine zilizopo Wilayani kwa lengo la kuhifadhi maliasili kwa kizaZi cha sasa na baadae.  Jumla ya Sh. 204,277,787 zimekusanywa na Wakala wa Misitu (TFS) katika shughuli mbalimbali za uhifadhi wa Maliasili.


SEKTA YA NISHATA YA UMEME 


DC Muro anasema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 ibara ya 63, Chama Cha Mapinduzi kinakusudia kuimalisha zaidi Sekta ya Nishati kuhakikisha kuwa Nchi inazalisha umeme wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda na soko la nje. 

Anasema katika kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ikungi imeendelea kusambaza umeme kwa Wananchi REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza ambapo walifanikiwa kupeleka umeme kwenye Vijiji 30. 

Anasema Miradi jazilizi (Densification) jumla ya Vijiji 6 vya Issuna, Mahambe, Puma – Jimbo, Ighuka – Masenku, Inyang’ongo – Makiungu na Mnang’ana – Dung’unyi vilipelekewa umeme.

“Miradi inayotekelezwa na TANESCO kupitia bajeti za ndani, jumla ya Miradi 12 ilitekelezwa ndani ya kipindi hiki cha Machi 2021 mpaka Machi 2022 yenye thamani ya Sh. 375,662,883.86” anasema Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga amewaomba madiwani wa wilaya hiyo kuendelea kusimamia ukamilishwaji wa miradi hiyo badala ya kuiachia Serikali na kuwa miradi hiyo Serikali imetoa fedha nyingi hivyo wanakila sababu ya kuisimamia kwa nguvu zao zote katika maeneo yao na akatumia nafasi hiyo ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa wito kwa Wananchi wa Wilaya hiyo kuitunza miradi hiyo kwani inamanufaa makubwa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za miradi katika wilaya hiyo na akatumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wote wa wilaya hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kutekeleza miradi hiyo kwa uaminifu mkubwa kwa kuanzia na Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, Watumishi, Wakuu wa Idara, Wataalamu pamoja na wananchi na Chama na akaomba ushirikiano huo uendelee ili Ikungi iwe mfano kwa maendeleo hapa nchini.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri katika hafla hiyo Leon Katanga alisema wataendelea kuwa tayari kusimamia sheria, taratibu na miongozo ya nchi yetu na kushiriki shughuli zote za kijamii na zile ambazo Chama na Serikali itaona zinaweza kufanywa na Halmashauri hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...