* Vyatajwa kuwa njia mbadala ya Elimu ya Sekondari, mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
Hayo yameeleza leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa taasisi ya 'Karibu Tanzania Organization' (KTO,) Maggid Mjengwa wakati wa ufungaji wa mafunzo maalum ya siku 5 kwa waratibu wa mafunzo, walezi wa wasichana, wakufunzi na wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 13 vinavyotekeleza programu ya Elimu Haina Mwisho ambayo ni mahususi kwa wanawake vijana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, ndoa za utotoni na umaskini pamoja na wale walioshindwa kuendelea na masomo ya sekondari ambao hupata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha na elimu ya ufundi.
Amesema ,jamii imeamka kutokana na mkazo wa Elimu hasa kwa wanawake uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasssan na taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi inawanufaisha vijana wa karibu kwa kuviunganisha vyuo hivyo na maeneo yaliyo karibu na miradi ili waweze kunufaika kiuchumi.
''Vijana wengi wamekuwa wakinufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kote nchini, vijana wamekuwa wakipata fursa za ufundi umeme na uchomeleaji katika miradi mikubwa ikiwemo REA na mradi wa uchimbaji wa madini ya Nickel mkoani Kagera...fursa hii ya kupata Elimu na ujuzi itumiwe vyema na vijana katika kujenga Taifa imara.'' Amesema.
Kuhusiana na mafunzo hayo Mjengwa amesema, ongezeko la vyuo 13 zaidi kutoka 41 na kufikia 54 ni kutokana na agizo la Serikali la kutaka vyuo vyote kudahili wanafunzi wa kundi hilo kupitia programu ya Elimu Haina Mwisho kuanzia Januari mwaka huu.
''Kupitia agizo hili tukaona ni vyema kukutana na wakufunzi, waratibu na walezi wa vyuo hivi 13 na kuwapatia mafunzo ya msingi,ujuzi, msaada ya kisaikolojia na changamoto za kukabiliana katika mchakato mzima wa kufanikisha safari ya mabinti wanaowahudumia.'' Amesema.
Ameeleza kuwa, mabinti wenye sifa za kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali wakiwa vyuoni kwa miaka miwili watasoma bila kulipa ada pamoja na kupata elimu ya sekondari na mafunzo ya ziada ambayo ni Elimu ya sekondari 50%, stadi za maisha 10%, ufundi na ujuzi 30% na Elimu ya ujasiriamali 10%.
''Wanafunzi wanachogharamia ni mahitaji binafsi ikiwemo nauli na mahitaji mengine ikiwemo taulo za kike ambazo bado ni changamoto na tunaangalia wadau waweze kusaidia eneo hilo.....Kuhusiana na chakula na malazi vyote vinagharamiwa na Serikali katika kuhakikisha kila mwanamke kijana anatimiza ndoto zake kielimu na kiuchumi.'' Amesema.
Kuhusiana na mabinti wa kike walio na watoto, Mjengwa amesema wanaweza kunufaika na programu hiyo kwa kuwa vyuo 34 kati ya 54 vina vituo vya malezi na makuzi ya watoto ambavyo watoto watapata huduma ya malezi katika vituo hivyo bure.
Kwa upande wake Lucy Ngasa mkufunzi kutoka chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija, Shinyanga amesema wamekuwa wakiwapokea na kuwapa elimu mabinti waliokatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali hasa mimba za utotoni.
''Mabinti wamepewa fursa hii adhimu kwa kuwa elimu haina mwisho...Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na KTO wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa kushirikiana na vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na sisi wakufunzi kwa kushirikiana na jamii tutatekeleza hili kwa kuhakikisha mabinti wa kike wanapata elimu na mafunzo ya stadi za maisha.'' Amesema.
Amesema kupitia mafunzo hayo ya namna ya kuishi na kuwahudumia mabinti hao yaliyotolewa na KTO yatawasaidia zaidi katika kuwajenga na kuwavuta mabinti wengi zaidi wanaodhani wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha baada ya kukatiza masomo yao.
Vilevile Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera, Kagera Shomari Mgombe amesema mafunzo hayo ya Programu wa Elimu Haina Mwisho kwa wakufunzi wa vyuo hivyo yamefika wakati muafaka ambao Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo katika suala la elimu hasa kwa mabinti wa kike ambao walikatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.
''Tukiwa kama wasimamizi wa taasisi tumejengewa uwezo wa namna bora ya kusimamia programu hii ya Elimu Haina Mwisho pamoja na kuwasaidia mabinti hawa ambapo katika chuo chetu tumeanza kuwapokea na mafunzo yanaendelea na udahili utaendelea hadi mwezi Aprili ....Hii ni fursa kubwa kwa mabinti ambao walikatisha masomo yao ya Sekondari, wajitokeze kujiunga ili waweze kupata elimu ya sekondari, mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya ujasiriamali.
Kuhusiana na namna wanavyoshirikiana na jamii katika kuwapata mabinti waliolengwa na programu ya Elimu Haina Mwisho mkufunzi kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija Shinyanga Mtambi Mussa amesema wamekuwa wakiangalia mahitaji katika jamii na kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali na wadau muhimu ambao ni KTO.
''Suala la mabinti kukatiza masomo kwa sababu za ujauzito na hali ngumu ya maisha jamii inataka kuona mabadiliko katika hilo, vyuo vyetu vina wajibu wa kusimamia hilo na kutekeleza majukumu kwa kutoa elimu iliyokatiza ndoto zao na mafunzo ya ziada ikiwemo mafunzo ya ufundi na tumekuwa tukishirikiana na viongozi wa dini katika kutangaza fursa hilo pamoja na kutembelea viongozi wa Kata na mitaa ambapo tumefanikisha kuwapata mabinti wengi walionufaika na programu hii.'' Amesema.
Amesema warsha hiyo iliyotolewa na KTO itawasaida kuwahudumia mabinti walioshindwa kumaliza elimu yao ya kidato cha nne kutokana na sababu mbalimbali kwa kutimiza ndoto zao na kupata ujuzi zaidi kupitia Elimu ya ufundi stadi ikiwemo ushonaji, ufundi wa umeme wa majumbani na mafunzo ya na ujasiriamali ambao hadi sasa yamewasaidia vijana wengi baada ya kuhitimu masomo yao.
Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyoshiriki mafunzo hayo ni Arnatouglu FDC's- Dar es Salaam, Bariadi FDCs- Simiyu, Buhangija FDCs- Shinyanga, Chala FDC's - Sumbawanga, Chilala FDC's - Lindi, Gera FDC's- Kagera, Kilosa FDC's- Morogoro, Kisangwa FDC's- Bunda, Msingi FDC's- Singida, Musoma FDC's- Mara, Nandembo FDC's- Tunduru, Tarime FDC's- Mara na Ulembwe FDC's kutoka Njombe.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija, Shinyanga Lucy Ngasa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo hayo na kueleza kuwa wataendelea kuwavuta mabinti wengi zaidi ili waweze kunufaika kwa kupata Elimu na ujuzi, Leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...