Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
WIZARA ya Afya imesema itashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufuatilia takwimu za wagonjwa wenye matatizo ya usikivu.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana kuhusu Siku ya Usikivu Duniani ambayo huadhimishwa Machi 3 kila mwaka.
Waziri Ummy alisema tatizo la wagonjwa wa usikivu kwa kiasi kikubwa lipo katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kwamba Serikali inajipanga kwa kushirikiana na NIMR kufuatilia ili iwe na takwimu sahihi.
"Endapo Serikali hatujajipanga na kuchukua hatua ifikapo mwaka 2050 idadi ya wagonjwa itaongezeka hivyo, tunaweka mikakati yetu wizara ya afya kujua takwimu sahihi,"alisema Waziri Ummy.
Aliwataka Watanzania kila mmoja kuchukua hatua kukabiliana na ugonjwa wa ukosefu wa usikivu kwani kwa kiasi kikubwa linasababishwa na mtindo wa maisha hasa vijana wanaoweka spika za kusikilizia masikioni kwa sauti kubwa bila kujali madhara yake.
Waziri Ummy pia aliagiza wajawazito wafike kliniki mapema kupima na kufuatilia afya zao ili kuepuka kujifungua watoto wenye matatizo ya ukosefu wa usikivu au uziwi.
Pia alitoa agizo akiwataka Watanzania waache tabia ya kutumia dawa bila kupewa ushauri wa daktari na kuwashauri wazazi waepuke kuwaadhibu watoto kwa kuwapiga vibao kwani wanaweza kusababisha kupata matatizo ya ukosefu wa usikivu.
Katika hatua nyingine alishauri watu wasikae sehemu zenye kelele nyingi pia wasitumie spika kuweka masikioni kwani zinachangia kuleta madhara ya usikivu.
"Tutakaa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kutoa maelekezo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hili," amesema Waziri Ummy.
Aidha alisema Serikali ina mikakati ya kuongeza madaktari bingwa wa masikio, pua na koo katika hospitali zote za rufaa 28 nchini sambamba na kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Fatma Kibao, amesema
Katika kuadhimisha Siku ya Usikivu Duniani hospitali hiyo inatoa bure huduma ya uchunguzi wa afya ya pua, koo na masikio.
"Kliniki ya magonjwa ya masikio, pua na koo katika hospitali yetu ilianzishwa mwaka 2020, tulianza na daktari bingwa mmoja na sasa tupo wawili. Kwa siku tunahudumia wagonjwa kati ya 15 hadi 21," alisema Dkt Fatma.
Daktari huyo aliiomba Serikali kuwawezesha kupata chumba cha kupimia usikivu ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Muhimbili ombi ambalo Waziri Ummy aliahidi kulifanyia kazi.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Bryson Kiwelu, alisema kati ya Januari 2020 hadi Januari 2022 wagonjwa 3,095 walihudumiwa katika kitengo cha koo, pua na masikio na kati yao 1,671 waligundulika kuwa na matatizo ya masikio.
Alisema pia wagonjwa 602 waligundulika kuwa na matatizo ya usikivu.
Waziri wa Afya , Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya usikivu Duniani yaliyo fanyika katika Hospitali ya Rufaa ya AmanaWaziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na Mganga Mkfawidhi wa Hospitali ya Amana Bryson Kiwelu mara baada ya kuwasili hospitalini hapo
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na Wagonjwa waliofika katika hema la matibabu ya Wagonjwa wa sikio ndani ya Hosptali ya Amana
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisikiliza kero za Wagonjwa aliowakuta katika eneo la OPD Ndani ya Hospitali ya Amana
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...