Na Mary Margwe, Simanjiro
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Dkt.Suleiman Serera ameahidi wananchi wa Kata ya Mirerani na Endiamtu kumaliza mgogoro wa ardhi wa shamba la Maro ndani ya mwezi mmoja, watakaobainika kuuza eneo kinyemela watakiona chamtema kuni, na kuzuia ekari 404.
Hayo amezungumza juzi mbele ya viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini, chama na serikali, kwenye mkutano wake unaoendelea wilayani humo wa kijiji kwa kijiji ambapo mwenyekiti wa CCM wilaya Omari Awadhi alikuwepo katika mkutano huo uliofanyika sokoni Mjini Mirerani.
Dkt.Serera alisema anajua wapo baadhi ya viongozi waliohusika katika mgogoro huo, taratibu zinaendelea ambapo
ametoa wiki moja kwa polisi kuchunguza suala hilo na kumpa jibu baada ya wiki moja na kuwachukulia hatua kali wote watakaowabaini wanahusika na kesi hiyo ya jinai, atakayebainika kuhusika na kuuza eneo hilo kwa maslahi yake atakachokutana nacho itakua fundisho kwake na viongozi wengine wengine wenye tabia kam yake.
" Nimewaagiza polisi kufungua jalada la mgogoro huu wa ardhi na kuwafungulia kesi mahakamani wahusika wote , kwani kuna mchezo mchafu umefanyika kwenye eneo la shamba la Maro hadi baadhi ya watu walionunua maeneo na kujenga nyumba zao kuwekewa alam ya X nikaagiza zifutwe," alisema Dk Serera.
Aidha amesema migogoro ya ardhi mingi inatokana na kuwepo kwa baadhi ya viongozi kusababisha ambapo pia amebaini kuuzwa kwa baadhi ya viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya watu walioathirika kwa kukumbwa na mafuriko yaliyotokea Mirerani mwaka 2018/2019, kwani amebaini wengi wao waliouziwa eneo hilo si walengwa wa mafuriko hayo, huku kuuzwa na pesa kuweka mifukoni mwa baadhi ya viongozi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani kinyume na utaratibu.
" Hili la shamba la Maro, ambalo mmelisema hapa na limeibuka kuwa ndio kero kubwa kwa wananchi wa Mirerani na Endiamtu, na hili niwahakikishie tu nitajitahidi, nilishaunda kamati fulani katika maeneo mengine mfano kule Okutu kulikua na shida kama hii nikaunda kamati ya vyombo vyangu vya ulinzi man usalama na hapa kwenye shamba la Maro nitafanya hivyo" alisema Dkt.Serera.
Aidha anafafanua kuwa shamba la Maro lilikua na ukubwa wa ekari zipato 373 Kama si 375 ambapo wananchi wengi walijitokeza kununua maeneo katika shamba hilo huku wapo waliouziwa na watoto wenyewe wa Maro, na wapo waliouziwa na baadhi ya viongozi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani na kupewa hati ambazo hazitambuliki na ofisi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, huku bila kujua kuwa hati zote za viwanja zinatolewa na ofisi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya na sio Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani.
Alisema mgogoro huo umemfikia takribani mwezi sasa umefika, ambapo alichukua uamuzi wa kuwaita hiyo familia ya Maro yenye mgogoro huo ambayo tayari ina kesi mahakama ya rufaa, kama inavyofahamika kuwa mali za familia huwa kuna wala wasimamizi wa mirathi, na hata wao wenyewe nao hawaongei, hivyo aliwaita kwa lengo la kuwasaidia na kuwapa busara fulani hivi licha ya kuwa haikuzingatiwa.
Aidha awali mkuu huyo alisema tayari familia ya Maro na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro walishakaa na kukubaliana kuwa katika ekari hizo kuwa wao wachukue asilimia 60 na adilimia 40 ichukue Halmashauri, sasa kilichoonekana hapa watoto wamejiuzia eneo kiholela huku bado wakitaka eneo lililobaki ligawanywe kwa kuchukua asilimia yao 60 wakati tayari walishalipunguza.
" Sasa hizo asilimia 40 ya Halmashauri itapatikana vipi, ni lazima nipite kwa kila mtu aliyejenga katika eneo lile ili nikuulize wewe uliyejenga ulilipataje hilo eneo , ukisema uliuziwa na watoto wa familia ya Maro maana yake ile asilimia yao 60 utakuja kuathiriwa na yale maeneo ambayo tayari wao wameyauza, sitakubali mtu ambaye tayari ameshakula keki yake akarudia tena kukata keki nyingine, kwasababu wanarudi nao sasa hivi wanataka ile asilimia ipimwe tu kwenye ekari 404 iliyobaki hilo siwezi kukubaliana nalo kabisa kwa maslahi mpana ya ninyi wenyeji wa Mirerani, Endiamtu na Simanjiro kwa ujumla, ndio maana hizo ekari 404 nimezizuia" alifafanua Dkt.Serera.
Aidha alisema zoezi hilo halitachukua muda mrefu kwasababu amelichukua mwenyewe, anataka kulifanyia kazi ikiwezekana ndani ya mwezi mmoja awe amelimaliza.
" Familia ya Maro niliwapa kazi ya kufanya lakini hawakuifanya kazi ile vizuri, hivyo nitawaita tena, ila niwaahidi tu wale ambao wamejenja zile alama ya X mlizowekewa zisiwape shida tulieni, nimepata meseji kuwa kuna mwenzenu anajiita katibu wa ile jumuiya yenu ametuma meseji kuwa akisema kuna ruhusa imetoka endeeeni , uchochezi kama huo ndio siutaki hakuna mtu niliyemtuma kufanya hivyo, nilichozuia mimi ni wale waliokuja kupiga alama ya X na nimewakataza akiwemo mwanasheria wa halmashauri kwasababu nilishamuonya yeye kibano chake ameshakipata kule ndio maana kazi nyingine haiendelei" aliongeza mkuu huyo.
Hata hivyo aliwasihi wananchi kutulia wakati serikali inaendelea kufanya kazi yake kwani yeye ndio mkuu wa wilaya hiyo yupo hapo kwa sababu ya kusimamia maslahi wakazi wa Simanjiro
Naye diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema ofisa ardhi wa mamlaka ya mji huo aliyejulikana kwa jina la Sullw, ameshirikiana na baadhi ya wenyeviti wa vitongoji kuuza ardhi ya eneo la shamba la Maro na kusababisha kuwepo kwa mgogoro huo.
"Huyu Sule na baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wameshirikiana kuuza ardhi ya wananchi na kuzua mgogoro unaorudisha nyuma maendeleo ya Kata yetu," amesema Salome.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia amesema baadhi ya wenyeviti wa vitongoji kwa tiketi ya CCM wenye uchu wa fedha wameuza kwa watu hata viwanja ambavyo ni mali CCM.
"Tunaonekana wabaya kwa sisi kukemea uuzaji ardhi wa holela, ila tunashukuru na mkuu wa wilaya kuingilia kati suala hili lililosumbua kwa muda mrefu" amesema Zacharia.
Hata hivyo, ofisa ardhi wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Sule amesema aliidhinisha uuzaji ardhi kupitia nyaraka za mamlaka hiyo baada ya muuzaji na mnunuzi kukubaliana, huku akisema alipewa idhini ya kuwapatia waanga wa mafuriko na aliyekua mkuu wa hiyo Mhandisi Chaula.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Dk.Suleiman Serera akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni moja ya ziara yake ya kijiji kwa kijiji inayoendelea wilayani humo, mkutano uliofanyika eneo la sokoni katika Mji Mdogo wa Mirerani, ambapo kero kubwa ilikua ni kuuzwa kwa viwanja katika shamba la Maro kinyume na utaratibu. Picha na Mary Margwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...