Na Mwandishi wetu
Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene , amesema kuwa kongamano la siku mbili la msaada wa kisheria ni sehemu muhimu itakayowaleta pamoja wadau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini ili kujadili utekelezaji wa sheria ya msaada wa kisheria na kuangalia namna ya kuboresha zaidi ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo lililofanyika Jijini Dodoma Machi 30 na kumalizika Machi 31 lililoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria na shirika la Legal Services Facility (LSF) lenye Kaulimbiu inayosema 'Msaada wa Sheria kwa Jamii yenye Haki na Jumuishi'
Waziri Simbachawene alisema kongamano hilo linalenga kuangazia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 kwa kuangalia mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa sheria hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita;
"Kabla ya kutungwa na kupitishwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017, wadau wa sekta hii hasa watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria walikuwa wakikumbana na changamoto nyingi kubwa ikiwa ni kutokutambuliwa katika taasisi mbalimbali za mifumo ya utoaji haki. Tunatarajia kusikia uzoefu wa wadau hawa na wengine baada ya sheria hii kuanza kutekelezwa"
Aidha Waziri Simbachawene alisema kongamano hilo linalenga kupata uzoefu wa utekelezaji sheria za msaada wa kisheria kwa kuangalia maeneo mengine ya nchi jirani kama vile KENYA, UGANDA na MALAWI huku lengo kuu likiwa ni kupata uzoefu na kujifunza kutoka kwa kila mmoja namna bora ya kukuza sekta hii muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Shirika la Legal Services Facility, Lulu Ng’wanakilala , amesema kuwa, kongamano la mwaka huu ni sehemu kubwa ya mafanikio ambayo LSF inajivua kwa kushirikiana na wadau wengine hasa serikali katika kuwezesha upatikanaji wa haki
"Tangu mwanzo LSF imekuwa mdau mkuu wa serikali katika kuhakikisha tunaendelea kufanya kazi kwa karibu katika kuwezesha upatikanaji wa haki ikiwemo kuchangia katika kuwezesha sheria ya msaada wa kisheria nchini Tanzania inapatikana."
Aliongeza kuwa "LSF kama shirika lisilo la kiserikali tumekuwa tukifanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kupitia uwezeshaji wa kisheria.
Uwepo wa sheria hii umekuwa nyenzo muhimu kwetu katika kuongeza upatikanaji wa haki kupitia wadau wetu wakubwa ambao wamekuwa wakitoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kwa watu wote hasa wanawake na wasichana"
Aidha Ng’wanakilala amesema, kongamano hilo ni muhimu sana na litawasaidia kufahamu kwa undani mafanikio changamoto na fursa ambazo zitaboresha upatikanaji wa Haki nchini;
"Kongamano ni muhimu sana katika kuinua sekta ya huduma za msaada wa kisheria kwani litatusaidia kufahamu kwa undani mafanikio, changamoto na fursa ya kukutoka na maazimio ambayo yataboresha upatikanaji wa haki nchini kwa ujumla hivyo tunafurahi sana kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika kuliandaa."
Naye Msajili wa Msaada wa Kisheria, Felistas Mushi amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano changamoto kubwa imekuwa ada ya usajili wa wasaidizi wa kisheria lakini hata hivyo serikali imeamua kufuta ada hiyo ili kuruhusu wasaidizi wa kisheria kujisajili kwa wingi zaidi.“Mpaka sasa tuna wasaidizi wa kisheria 757 ambao wamejisajili katika mfumo wa serikali kama watoa huduma za mnsaada wa kisheria. Vilevile tuna mashirika 202 tu ya wasaidizi wa kisheria yaliyosajiliwa baada ya kukidhi vigezo. Kuanzia mwaka mwezi wa pili ada hizo ambazo zilionekana ni kikwazo zimefutwa kabisa”
Mbali na uzinduzi wa kongamano hilo la siku mbili la msaada wa kisheria jijini Dodoma kuanzia Machi 30-31,2022 pia kulifanyika uzinduzi wa ripoti maalumu ya wadau wa upatikanaji Haki nchini Tanzania (LSF Access to Justice Stakeholders Mapping Report), Meneja Programu wa LSF, Deogratias Bwire amesema wamefanga Utafiti na kuja na ripoti hiyo muhimu kwa wadau wa upatikanaji wa haki nchini ambapo ripoti imebabainisha kuwa miongoni mwa wadau wakubwa katika Utoaji huduma za msaada wa kisheria ni wasaidizi wa kisheria, Mahakama, Polisi, viongozi wa serikali, viongozi wa dini bila kusahau viongozi wa kimila.
Bwire aliongeza kuwa Ripoti hii inaonyesha kama wadau wote wataunganisha nguvu ya pamoja kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha zaidi upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Pia mdau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini, John Nginga asema Serikali pamoja na Asasi za kiraia nchini walifanya kazi kubwa kuhakikisha sheria hiyo inakuwepo. Kupitia kongamano hili, ni matumaini wadau watajadili vyema na kutoa michango bora yenye lengo la kuboresha sekta hiyo kupitia utekelezaji wa sheria.
Ikumbukwe kuwa Kongamano hilo limewaleta pamoja Taasisi za Serikali, Asasi zisizo za kiserikali (CSO) ,Wadau wa maendeleo na wadau mbalimbali takribani 120 wanaojihusisha na utoaji wa msaada wa sheria kutoka Tanzania bara na Zanzibar, kujadili na kutathmini utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Sheria ya Mwaka 2017.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...