Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania kutunza mazingira, hususan uoto wa asili kwa kuepuka kukata au kuchoma miti ovyo.

Mhe. Rais ametoa wito huo leo wakati akihutubia katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji kilichofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amesema katika maeneo ya vijijini, chemichemi nyingi za maji pamoja na baadhi ya mito imetoweka kutokana na uharibifu wa mazingira, na pia kutokana na kufanya shughuli nyingine za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji.

Aidha, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Maji kufanya utafiti na kuangalia uwezekano wa kutumia maji ya Mto Rufiji kwa ajili ya matumizi ya baadae katika jiji la Dar es Salaam.

Awali akizindua mradi wa maji uliogharimu shilingi Bilioni 18 utakaosambaza maji kutoka Mboga, Chalinze hadi Mlandizi Wilayani Bagamoyo, Rais Samia ameikopesha Wizara ya Maji shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi ili yaweze kuwafikia kwa haraka.

Pia, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuhakikisha wanalipa ankara za huduma ya maji wanayopatiwa ili Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Dar es Salaam (DAWASA) iendelee kutoa huduma kwao.

Vile vile, Rais Samia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuweka mikakati ya kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza Mkoani humo kwa kuhakikisha kuwa wanatenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji.

Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia Mhe. Ahmed Abdulazizi Kattan Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili hususan katika masuala ya uwekezaji.


ZuhuraYunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...