Na Khadija Kalili

Serikali imeipongeza Clouds Media Group kwa kuendesha programu ya Malkia wa Nguvu yenye kauli mbiu 'Tupo Site' na kuwapa moyo wale wanawake wajasirimali wanaoendesha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali kwenye jamii.

Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo za Malkia wa Nguvu zilizotolewa usiku wa kumkia tarehe 27/03/2022 zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Clouds imekuwa ikiiunga mkono serikali kwa muda mrefu hivyo wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kutokana na mchango mkubwa ambao Clouds wamekuwa wakitoa kwa jamii.

Waziri Dkt Gwajima amesema hapa nchini wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wetu ambapo kitaifa asilimia themanini (80%) ya nguvu kazi ya sekta ya kilimo ni wanawake na wanawake hawa huzalisha asilimia sitini (60%) ya chakula chote hapa nchini.

“Katika baadhi ya familia, wanawake ndiyo wahimili wakuu kwa maana ya upatikanaji wa chakula, mavazi na huduma nyingine za kijamii zikiwemo za kuwapeleka watoto shule na za afya kwa maana ya kuwahudumia wanafamilia ambao ni wagonjwa”. alisema Waziri Dkt.Gwajima.

Alisema kuwa pamoja na mchango mkubwa wa wanawake kwenye maendeleo ya jamii, nchini Tanzania na katika nchi nyingine duniani wanawake wanaendelea kukabiliana na changamoto ya kuwa na uchumi duni ikilinganishwa na wanaume jambo ambalo siyo haki.

Aidha alisema Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 62.68 katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya Mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri zote nchini ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2021 jumla ya Shilingi bilioni 53.81 zilikopeshwa kwa Vikundi 7,993 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu sawa na 86%. Kati ya fedha hizo shilingi Bil. 28.17 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake 4,894 vilivyozalisha ajira 52,428.

Pamoja na hayo Waziri Gwajima amesema Serikali inampango wa kuondoa kero kwa wajasiriamali wakiwemo Wajane, lishe na wauza mbogamboga kwa kupatiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara yenye ukubwa wa hekta 15,822.64 katika Halmashauri 150 nchini.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa (Sensa) kwani ni muhimu kwa kupata takwimu sahihi za watu na makazi ili kuwezesha Serikali kufanya makisio na kupanga mapato na matumizi katika shughuli za serikali.

“Wanawake ni kundi ambalo tunatakiwa kuwa mbele kuitikia zoezi la sensa mwaka huu wa 2022 na tuwaelimishe na wenzetu ili nao waweze kushiriki zoezi hili ambalo ni muhimu kwa taifa kwa ujumla”. Amesema

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Clouds Media Group Joseph Kussaga amewapongeza watumishi wote wa Clouds Media Group kuhakikisha inawapa kipaumbele wanawake kwenye kazi na kufanya tamasha hilo kuwa kubwa na lakihistoria hapa nchini.

“Zamani mimi na marehemu Ruge tulikuwa hatuwezi kulala tukamuachie mtu kazi, ila leo nalala kabisaaaa, nakuja kwenye shughuli nakuta show imesimama vizuri” alisema Kussaga.

Kilele Cha Malkia wa Nguvu kilikwenda sambamba na utoaji wa Tunzo ambapo walimpatia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliyeshukuru kwa kupatiwa tunzo hiyo huku akisema kuwa hakuwahi kufikiria kama ipo siku angetunukiwa.


Wengine waliopata tunzo hizo ni kikundi Cha wasichana Cha Malkia ajae Cha Lilian Production Group', tunzo ya Kilimo Biashara ilikwenda kwa kina mama Goba Mushrooms,Afya na Ustawi wa Jamii ilikwenda kwa wanawake wafanya usafi kutoka Kata ya Miburani,Kwa upande wa Sayansi na Teknolojia ilikwenda kwa Kikundi Cha Wajane ambao wanafyatua matofali,Tunzo ya Muziki ilikwenda kwa Ritha Paulsen na wengine wengi waliweza kung"ara akiwemo Malkia Muongoza Ndege Mwanajumaa Kombo.


Pia wasanii maarudu kama Juma Jux, Maua Sama, Isha Mashauzi nawengineo walipamba usiku huo.






 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...