Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO -19 imetenga shilingi bilioni 1.01 kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo waongoza watalii wanawake takribani 1060 nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa kuhitimisha mafunzo ya waongoza Watalii wanawake 89 yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Mafunzo haya ni mahususi kwa wanawake kama jitihada za makusudi kabisa za Serikali kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa za kuchangia katika maendeleo ya nchi kupitia utalii na kunufaika kupitia sekta hiyo” ” amefafanua Mhe. Masanja.
Amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza vyema Tanzania ndani na nje ya nchi.
“Natambua mmekuwa mabalozi muhimu mnaotegemewa kuiuza nchi yetu hivyo sifa ya kwanza mnayotakiwa kuwa nayo ni uzalendo. Wageni mnaowapokea wana sifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa hivyo wakati mnatekeleza majukumu yenu mnapaswa kuwa na uelewa mpana wa shughuli za utalii na pia muwe na maadili, weledi na uadilifu”amesema Mhe. Masanja.
Aidha, amewaasa waongoza watalii hao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watalii wanapowasili nchini ili kujenga taswira nzuri ya Tanzania na kumfanya mtalii aweze kurudi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo waongoza watalii wanawake yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya waongoza watalii wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(hayupo pichani) wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...