Adeladius Makwega-DODOMA.
Vita baina ya Ukraine na Urusi vinaendelea huku hali ya uharibifu hasa kwa upande wa Ukraine ikishika kasi. Nayo namba ya binadamu wanaopoteza maisha ikiongezeka, iwe askari wenye mitutu vitani ama raia wanaohangaika kuponya nafsi zao.
Kama nilivyotilia maanani matini yangu ya kwanza juu ya Ukraine itashinda vita kisiasa bado natilia maanani dhana hii ya ushindi wa vita vya kisiasa. Kabla sijaingia katika kiini cha matini yangu ya leo, naomba nikukumbushe jambo moja kuwa Ujerumani na washirika wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walishindwa vita hivyo.
Huku taifa hilo likipitia hatua kadhaa ngumu lakini sasa ni zaidi ya miaka 80 ya vita hivyo, Je hali ya Ujerumani ikoje? Hususani maendeleo ya raia wake hasa mtu mmoja mmoja.
Hivi tunavyozungumza upatikanaji wa elimu, bima za afya, malipo kwa wasio na ajira, miundo mbinu ya taifa hilo ni bora na imara sana na hata maamuzi yake katika masuala ya kimataifa wanajiamulia misimamo yao wenyewe bila shuruti la taifa lingine.
Matarajio ya wengi, Ujerumani kwa kuwa walihusika moja kwa moja katika vita hivyo pengine wangekuwa miongoni mwa taifa dhoofu li hali zaidi lakini sasa mambo yameguka.
Kuutilia maanani ushindi wa huu wa kisiasa, mwaka 1956 kulikuwa na mgogoro baina ya Uingereza na Misri, chanzo kilikuwa ni juu ya Mfereji wa Suez kwani Uingereza, Ufaransa na Israel waliungana na kupambana na Misri huku wakishambulia Mji wa Port Said.
Muungano huo wa ushirika wa kuishambulia Misri ulitokana na namna Rais wa Misri wakati huo Gamal Abdel Nasser kwa kuutaifisha Mfereji wa Suez uliokuwa chini ya imaya ya Ufaransa na Uingereza kila mmoja akiwa na hisa zake.
Hali hii ilikuwa kama ilivyofanyika Tanzania mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha. ambapo mali kadhaa zilitaifishwa.
Jambo hlo liliwakwaza mno Waingereza chini ya Waziri wao Mkuu wa wakati huo Antony Eden. Vifaa kadhaa za kijeshi vya washirika hao vilisogezwa jirani na Misri tayari kwa mapambano.
Wababe hao walianza kuchapana huku meli zaidi ya 40 za Uingereza, Ufaransa na Israel zilishambuliwa na kuzamishwa baharini. Wakati uwanja wa mapambano moto ukiwaka, Marekani chini ya Rais Dwight D Eisenhower, Umoja wa Usovieti na Umoja wa Mataifa kwa pamoja waliwaomba Waingereza kuyaondoa majeshi yao jirani na Mji wa Port Said.
Wakati huo hawa Umoja wa Mataifa walikuwa bado wanakumbuka vizuri athari ya Vita vya Pili vya Dunia. Huku Waziri Mkuu wa Canada wakati huo Lesser Pearson akijitoa mhanga kuutatua mgogoro huo chembe kwa chembe hadi upepo mbaya ukapita salama. Lakini Uingereza ikiwa wamepokonywa Mfereji wa Suez na taifa ambalo hawakutegemea lingeweza kufanya hivyo.
Msomaji wa matini hii tambua kuwa kabla ya Julai 26, 1956 Mfereji wa Suezi ulikuwa ukimilikiwa kwa pamoja baina ya Uingereza na Ufaransa kama nilivyokudokeza hapo juu. Kuutafisha mfereji huo na kurudi kuwa mali ya Misri ilikuwa ni sawa nakuchezea sharubu za Simba aliye mawindoni lakini Rais Kijana wa Misri wakati huo Gamel Abdel Nasser aliweza na kushinda chemsha bongo hiyo.
Umoja wa Mataifa ukaamua kuwa tangu oktoba 1956 hadi machi 1957 kutokana na mgogoro huo wakawekwa polisi maalumu kulinda eneo hilo na mpaka baina ya Misri na Israel ili kuhakikisha kimbunga cha mgogoro huo kinatulia.
Mara baada ya vita hivyo Misri ilishinda kisiasa na jambo hilo liliwaumiza mno Waingereza huku wakitumia pesa nyingi kupambana vita hivyo na bado mfereji huu ukichukuliwa na Misri.
Kwa hiyo vita vikahama kutoka uwanjani jirani na Port Said wakitumia bunduki, mabomu na mizinga vikiwa vita vya maneno kwa kutumia vyombo vya habari likiwamo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Gamal Abdel Nasser kwa kuwa alikuwa kiongozi mwerevu mno, mjanja, mzungumzaji mzuri na mwenye kujua kuyatumia maneno pahala panapotakiwa aliyajibu mapigo hayo huku akishangilia ushindi wa taifa lake kubaki na Mfereji wa Suez.
Akizungumza na viongozi kadhaa wa taifa hilo Rais Nasser alisema kuwa BBC walirusha makala juu ya Yemeni, wakienda mbali zaidi kwa kudai kuwa kuwa waliwatusi viongozi kadhaa wa Misri na Yemen akisema kuwa sasa si wakati sahihi wa kuyajibu matusi hayo.
Rais Nasser alisema kuwa Uingereza ilitumia zaidi ya paundi milioni 100 katika mgogoro huo na haikupata kitu huku majeshi ya Misri yakiwashinda Waingereza na washirika wake.
“Kama wakisema Gamal Abdel Nasser ni mbwa basi wao ni watoto wa mbwa. Lakini wakifanya hivi kwetu, wataweza kufanya haya haya kwa kwa mataifa ya ulimwengu wa tatu , kwa mataifa ya ulimwengu wa nne na hata mataifa ya ulimwengu wa tano.”
Hali ilikuwa tete huko Uingereza, Waziri Mkuu wake wa wakati huo Antony Eden kujiuzulu. Nayo nyota ya jaa ikiangukia huko Canada ambapo Waziri Mkuu wake wa wakati huo Lesster Pearson alishinda tuzo ya amani ya Nobel kwa utatuzi wa mgogoro huu wa Mfereji wa Suezi, kwa hakika kufa kufaana.
Tangu wakati huo hali ya Uingereza kutazamwa kama taifa lenye nguvu ikaanza kuondoka kwa kasi mithili ya theruji inayoyeyuka katika jua kali.
Msomaji wa matini zangu umeona namna ya mataifa haya mawili ya Ujerumani na Misri namna yalivyonufaika na ushindi wa vita vya kisiasa ?
Mwanakwetu kwa leo naweka kalamu yangu chini kwa kusema bayana kuwa hakuna jambo, narudia hakuna jambo la muhimu mno kwa taifa lolote lile likiwa vitani kama kushinda vita vya kisiasa.
Je niendelee na matini za migogoro ya kimataifa au nibake na changamoto zetu za hapa nyumbani Tanzania?
Nasubiri jibu lako
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...