Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Ridhiwani Kikwete ameendelea na ziara ya Jimbo ambapo amepokea kero sugu ya ardhi zilizohodhiwa pasipo kuendelezwa katika kata ya Vigwaza .
Akiwa kwenye ziara hiyo amefanya mikutano mitatu mikubwa katika Vijiji vya Buyuni, Kwazoka na Vigwaza Kambini na akiwa Kwazoka Wananchi waliiomba Serikali kurejesha eneo la Hekta 280 ambalo limeshindwa kuendelezwa na Mwekezaji wa Machine Consultant Ltd (BARUTI) ambao walipewa eneo hilo toka mwaka 1992 kwa ajili ya kufanyia uwekezaji .
Walisema ni miaka 30 mpaka sasa hawajaweza kufanya uwekezaji hivyo wanaiomba Serikali kuangalia namna ya kurudisha eneo hilo ili Wananchi walitumie kwa maendeleo maana Wawekezaji hao wameonyesha waziwazi kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu .
Kwa upande wake Ridhiwani amewaagiza Wataalamu wa Ardhi wa Chalinze kuona namna ya kuishauri Wizara yake ili eneo hilo lifutwe na kurudishwa kwa Wananchi kwa matumizi ya maendeleo maana kwasasa limekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.
Kuhusu kero ya mgogoro mkubwa wa Ardhi aliyolalamikiwa na Wananchi eneo la Kiloweko na kati ya Kwazoka na Chaulu,Ridhiwani alisema anakwenda kuyafanyia kazi na kuwaahidi Wananchi kurudisha majibu haraka iwezekanavyo.
Migogoro mingine mikubwa ya ardhi aliyoelezwa Ridhiwani akiwa katika Kijiji cha Vigwaza Kambini ni pamoja na ule wa kati ya Kijiji cha Vigwaza na Visenzi na Vigwaza na Mnindi ambapo alitoa maelekezo kwa Wataalamu wake wa Wizara kufika maeneo hayo kumaliza migogoro hiyo.
Ridhiwani pia alitumia mikutano hiyo kuwaeleza Wananchi kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Rais Samia kupeleka fedha katika Wilaya ya Chalinze kutekeleza miradi mikubwa ya elimu, miundombinu, afya, umeme, upimaji na urasimishaji ardhi, kusaidia vikundi vya Wajasiriamali wadogo kupata mikopo .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...