Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Absa imeahidi kuendelea kutoa mchango wake kwa mashindano ya mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kupitia udhamini wake, ambapo pia itao hakikisho la wafanyakazi wake kuendelea kushiriki mbio.
Akizungumza hayo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya 20 ya mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa Kampuni ya Absa, Aron Luhanga alisema tukio hilo ni jukwaa zuri kwa wafanyakazi wa Benki hiyo kushirikiana na watu wengine sambamba na kutafuta soko zaidi kwa ajili ya bidhaa zinatolewa na taasisi hiyo ya kifedha.
"Lengo letu ni kuhakikisha wafanyakazi wetu wanaimarisha afya zao na ndiyo maana huwa tunawahimiza wawe wanashiriki matukio kama hili mara kwa mara”, alisema na kuongeza kuwa Absa imekuwa ikiwafadhili wafanyikazi wake kushiriki matukio ya aina hiyo na kuhakikisha wanajiandaa vyema kabla ya ushiriki huo.
Kuhusu mbio za Kilimanjaro marathon ambayo hufanyika mjini Moshi kila mwaka na kushirikisha zaidi ya wanamichezo 12,000, Luhanga alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mashindano hayo muhimu kupitia ufadhili wake.
Absa ni mmoja wa wadhamini waliopongezwa na mgeni rasmi katika mbio hizo mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, ambapo aliisifu benki hiyo kwa mchango wake mkubwa kama moja ya wadhamini wa mashindano hayo.
Mbali na udhamini wake, banda la benki ya Absa lililokuwa kwenye maonyesho yaliyofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na kushirikisha wadhamini wengine, lilikuwa kivutio kwa washiriki na wageni wengine mbalimbali wa mbio hizo.
Aidha wafanyakazi wa taasisi hiyo walioshiriki mbio hizo walionekana wenye furaha tele huku wakipiga picha na kufurahia nyakati hizo nzuri pamoja.
"Wafanyikazi wetu, wanafamilia na marafiki zao wamekuwa na wakati mzuri wakati uongozi wa benki ulipowakarisha hapa; Wapo walioshiriki mbio hizo huku wengine wakiwa watazamaji”, alisema na kuongeza kuwa wanajivunia kuwa sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 20 ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon.
Kwa mujibu wa Luhanga, mbali na ushiriki huo, benki ya Absa pia ilikuwa mdhamini wa meza za maji kwa ajili ya washiriki wa mbio hizo zilizokuwa zimewekwa maeneo mbalimbali ya njia zilizotumiwa na washiriki wa mbio hizo.
Mbali na Absa Bank, wadhamini wengine wa mbio hizo ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager- Mdhamini Mkuu, Tigo- 21km, Grand Malt -5km. Wadhamini wa meza ya maji- Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water na wasambazaji rasmi, GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, Surveyed Plots Company Ltd, Bodi ya Utalii Tanzania na CMC Automobiles.
Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...