Na Eleuteri Mangi - WUSM

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) wametoa tuzo kwa wanafunzi watatu wa shule ya Sekondari ya Kongwa ambao wameandika insha kuhusu mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika.

Akikabidhi tuzo kwa wanafunzi hao wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, ambayo yamefanyika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma Machi 23, 2022, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema tuzo hizo zinaonesha ushiriki mkubwa wa wanafunzi katika kujifunza na kujua historia ya nchi yao.

Wanafunzi ambao wamepata tuzo ni Spinola Dismasi Kihoo ambaye ameandika insha inayohusu mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, Nicolaus Mahaka Mhowele ameandika insha inayohusu mchango wa Kongwa katika Ukombozi wa Bara la Afrika na Anie Steven Chung’umba ambaye ameandika insha a inayohusu mchango wa Kongwa katika Ukombozi wa Bara la Afrika.

“Nimewiwa kuanza kwa hisia kutokana na uzalendo uliotukuka wa viongozi wetu walioutoa wakati wa harakati hizi za ukombozi wa Afrika, ninapowaona wanangu hapa wanafunzi, ni matamanio yangu mkue katika uzalendo, maadili, umoja, upendo na mshikamano ambavyo ndiyo vilikuwa chachu na nguzo wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

Wanafunzi hao wameonesha umahiri wao wa kuandika insha kuhusu fani za ubunifu, Sanaa na Utamaduni zenye maudhui ya mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika, tuzo hizo zimetolewa katika maeneo mawili ya insha bora kuhusu mchango wa eneo la Kongwa katika Ukombozi wa Bara la Afrika na mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Akitoa taarifa ya Programu ya Urithi wa Ukombozi Afrika, Mratibu wa Programu hiyo Bw. Boniface Kadili amesema kuwa wanafunzi hao wamekuwa chachu ya kujua historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo taasisi yake imejikita kutambua maeneo yote ya kiukombozi ikiwemo vielelezo vilivyotumika wakati huo ili viweze kuhifadhiwa kisasa viweze kutumika kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo hapa nchini na duniani kote.

Bw. Kadili ameongeza kuwa ni dhahiri wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Kongwa ni miongoni mwa wanafunzi nchini wanaonufaika na elimu ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuwa wanasoma katika eneo ambalo wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika waliyatumia kuzikomboa nchi zao.

Washindi wa shindano hilo wamepatikana baada ya wanafunzi 120 kushiriki kuandika insha ambazo nane ndizo zilikidhi vigezo vilivyowekwa na WIPO na hatimaye wanafunzi watatu kuibuka kidedea kwa uandishi ulioeleza vilivyo historia ya eneo la Kongwa.

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (wa pili kushoto) akimkabidhi tuzo kwa mwanafunzi Spinola Dismasi Kihoo kutoka shule ya Sekondari Kongwa ambaye ameandika insha inayohusu mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika ambayo yamefanyika Machi 23, 2022, wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (wa pili kushoto) akimkabidhi tuzo kwa mwanafunzi Anie Steven Chung’umba kutoka shule ya Sekondari Kongwa ambaye ameandika insha ambayo pia inahusu mchango wa Kongwa katika Ukombozi wa Bara la Afrika wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika ambayo yamefanyika Machi 23, 2022, wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...