*Wakubaliana kuimarisha ushirikiano wa biashara ili kukuza uchumi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Khalid bin Khalifa bin Abdulaziz Al Thani ambapo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara ili kukuza uchumi.
“Ninamuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika vikao vyenye lengo la kuimarisha mahusiano kati ya nchi ya Tanzania na Qatar na tumepata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Qatar.”
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Machi 22, 2022) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Khalid bin Khalifa bin Abdulaziz Al-Thani katika Ofisi ya Waziri Mkuu huyo iliyopo Doha,Qatar.
Amesema moja kati ya jambo kubwa walilolijadili ni uimarishwaji wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuongeza wigo wa maeneo mengi zaidi ya ushirikiano baina ya mataifa hayo na hivyo, kutumia vema fursa ya kuwa na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia kwa miaka mingi.
Waziri Mkuu amesema kuwa kati ya mambo waliyoyawekea msisitizo ni pamoja na kuimarisha biashara kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Chemba ya Biashara ya Tanzania kupitia ushirikiano na wenzao wa Qatar na kwamba shughuli hizo zitaratibiwa na wizara husika ili kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa.
Amesema hivi karibuni kutakuwa na kikao cha pamoja cha wafanyabiashara wa Qatar ambao wameonesha nia ya kuja nchini Tanzania. Hivyo, Serikali itawasimamia na kuwakutanisha na timu ya wafanyabiashara wa Tanzania kupitia TPSF ili wapate nafasi ya kujadiliana maeneo mengi ya uwekezaji.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na kuimarisha mahusiano katika maeneo ya kibiashara na kisiasa pia viongozi hao wamekubaliana kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya elimu ambapo wanafunzi wa Tanzania watapata fursa ya kwenda kusoma Qatar na wa Qatar watakuja kusoma nchini.
“Tunaendelea kuweka msisitizo wa ushirikiano kwenye maeneo ambayo yatatukuzia uchumi zaidi likiwemo eneo la utalii ambapo tunapata watalii wengi kutoka Qatar kupitia shirika la ndege la Qatar ambalo linaleta watalii wengi wanaopenda kuja kuona hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti, Mlima Kilimanjaro pamoja na Visiwa vya Zanzibar.”
Amesema maeneo mengine yaliyowekewa msisitizo katika mazungumzo hayo ni ya sekta za madini na kilimo ili kuhakikisha maeneo hayo ya uzalishaji yanapata wawekezaji wengi. “Pia Tanzania ni nchi ya pili yenye mifugo mingi Afrika, hivyo tumewaalika Wa-Qatar waje wawekeze kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ili tupate soko la bidhaa hizo.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 22, 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...