Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imeanza maandalizi ya ukarabati wa barabara kuu ya Mwanza – Shinyanga yenye urefu wa kilometa 104 ambao utahusisha upanuzi wa barabara hiyo kutoka njia mbili hadi njia nne sehemu ya Mwanza Mjini – Usagara yenye urefu wa kilometa 25.
Akijibu swali Bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Nyamagana, Mhe. Stanslaus Mabula, Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Kasekenya amesisitiza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hiyo iko katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika baadae mwezi huu.
Amesema baada ya usanifu wa kina kukamilika na gharama za ukarabati kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati utakaohusisha upanuzi wa barabara hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, amesema ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa, Shirika la Reli Tanzania (TRC), inakarabati mabehewa 37 ili kuimarisha huduma ya usafiri wa treni mkoani Kigoma.
Mhe. Mwakibete alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kilumbe Ng’enda, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuboresha usafiri wa Reli ya Kigoma – Dar es Salaam ambao umekuwa ukifanya safari mbili kwa wiki badala ya safari moja kila siku kama ilivyokuwa awali.
Naibu Waziri Mwakibete, amelihakikishia Bunge kuwa Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria na baada ya utekelezaji wa kazi hizo, idadi ya safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma zitaongezeka kutoka safari mbili hadi nne kwa wiki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...