Na WAF - DSM
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji wakiwemo wajawazito na wagonjwa wa ajali.
Dkt. Mollell ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua kampeni ya uchangiaji damu salama katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
"Damu haiuzwi, damu haiwezi kutengenezwa zaidi ya wananchi wenyewe kujitolea, hivyo tunawaomba wananchi wajitokeze kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu." Amesema.
"Tunapoteza wagonjwa wengi wakiwemo wanaopata ajali pamoja na wajawazito kwasababu ya uhaba wa damu salama, hivyo rai yangu kwa Watanzania kujenga tabia ya kuchangia damu" Amesisitiza Dkt. Mollel.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ameelekeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuboresha huduma kwa mteja (customer service) kuanzia mgonjwa anapoingia getini, anapopata huduma mpaka anapomaliza kupata huduma ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.
Amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo ni juu yetu sasa kama Wizara kuboresha huduma kwa mteja.
Katika hatua nyingine Dkt. Mollel amewataka Wataalamu kuwekeza katika tafiti za magonjwa mbalimbali ili kuja na majibu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko na kuwasaidia wananchi.
Nae Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema, elimu ya kutosha itolewe ili kila mmoja aone umuhimu wa kuchangia damu na kumsaidia mtu yeyote ili damu salama ipatikane kwa wakati na saa 24 katika vituo vyote vya kutolea huduma kwani serikali imenunua vifuko vya kuhifadhia damu.
‘’Kila Mkoa utengeneze mpango wake wa kuhakikisha upatikanaji wa damu salama unafanyika kisha muwasiliane na wizara kwani jukumu lililopo ni kutoa elimu na kuhakikisha damu ipo katika vituo vya kutolea huduma,’’ alisisitiza Dk Sichwele.
Mbali na hayo Dkt. Sichalwe amesema, mchango wa Chuo cha Muhimbili katika kuboresha huduma ni muhimu sana kwasababu ndio sehemu ambayo inapika watoa huduma wengi wakiwemo madaktari, hivyo kama Wizara tunathamini sana mchango huo.
Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Damu salama Dkt. Magdalena Lyimo amesema, mwaka jana Mpango umefanikiwa kukusanya chupa 331,279, na kuweka wazi kuwa bado mahitaji ni mengi, hivyo kuwaasa wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji.
Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uchangiaji damu katika Chuo Kikuu cha Afya Shirikirishi Muhimbili
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akisema jambo wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uchangiaji damu katika Chuo Kikuu cha Afya Shirikirishi Muhimbili.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akisema jambo wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uchangiaji damu katika Chuo Kikuu cha Afya Shirikirishi Muhimbili
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt. Magdalena Lyimo akisema jambo wakati wa ufunguzi wa kampeni ya uchangiaji damu katika Chuo Kikuu cha Afya Shirikirishi Muhimbili.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri w afya Dkt. Godwin Mollel pamoja na Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Afya, Wataalam wa Afya pamoja na Wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
Picha ya pamoja Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiwa na viongozi wa Taasisi za Wizara, Wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sanyansi Shirikishi pamoja na wanafunzi wachangia damu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...