Na Mbaraka Kambona, Tanga
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali
imeweka mipango mizuri ya kuhakikisha kijiji cha Msomera kilichopo
Wilayani Handeni, Mkoani Tanga kinakuwa na miundombinu ya kisasa ya
kuhudumia mifugo ikiwemo Majosho, Malambo na Nyanda za malisho ili
wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro watakaohamia katika eneo hilo
waweze kufuga kisasa na kwa tija.
Ulega aliyasema hayo Aprili
11, 2022 alipofanya ziara katika Kijiji hicho cha Msomera ambapo kuna
eneo limetengwa maalum kwa ajili ya wafugaji kutoka katika eneo la
hifadhi ya Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari yao ili kuendeleza shughuli
zao za ufugaji.
Baada ya kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili
ya Malisho, Majosho na Malambo, Mhe. Ulega alitoa maelekezo kwa Wataalam
wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuweka mikakati mizuri ya
kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo ili wafugaji hao kutoka
ngorongoro watakapohamia eneo hilo wakute miundombinu ipo tayari na
waweze kuendelea na shughuli zao.
“Tunataka wafugaji watakaokuja
kufanya shughuli zao katika kijiji hiki cha msomera, wafanye shughuli
zao za ufugaji kisasa, wafanye ufugaji wa kibiashara na tunataka hapa
pawe ni shamba darasa ili hata mtu akitaka kujifunza ufugaji wa kisasa
aletwe hapa”,alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pesa kwa
ajili ya kujengwa Majosho kumi (10) Wilayani humo ili mifugo iweze
kuhudumiwa vizuri huku akisisitiza kuwa ufugaji huo wa kisasa
utakaofanywa kijijini hapo utasaidia viwanda hapa nchini kupata
malighafi bora na za uhakika.
Mhe. Ulega aliwataka watendaji hao
wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuwa na mkakati wa pamoja ambao
utaonesha utendaji wa shughuli zao kwa kila wiki na wawe wanaanda
taarifa na kuzipeleka katika mamlaka husika.
Aidha, alitumia
nafasi hiyo pia kuwahimiza wafugaji watakaohamia Wilayani hapo kuwa
tayari kubadilika na kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufgaji wa
mazoea ambao wamerithi kutoka kwa wazee wao kwani kwa sasa tija yake ni
ndogo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe
alisema kuwa ujio wa Naibu Waziri Ulega Wilayani humo ni faraja kwao na
anaamini utasaidia kutoa msukumo kwa Wataalam kuongeza nguvu katika
utendaji hususan katika sekta ya mifugo.
Aliongeza kwa kusema
kwa sasa kipato cha mwananchi wa kawaida wilayani humo ni kiasi cha
shilingi laki nane na kumi kwa mwaka (810,000) lakini wamejiwekea
malengo kuwa ifikapo mwaka 2025 kipato hicho kiongezeke kufikia shilingi
Milioni moja (1000,000) kwa mwaka na hiyo itafanikiwa kupitia shughuli
za ufugaji wa kisasa unaotegemewa kufanyika katika kijiji cha Msomera.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Msaidizi wa Mradi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdallah Fedes (kulia) kuhusu ramani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya wafugaji kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro wakati wa ziara yake ya kukagua eneo hilo lililopo katika Kijiji cha Msomera, Wilayani Handeni, Mkoani Tanga Aprili 11, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(watatu kutoka kushoto) akikagua moja ya eneo ambalo litatumika kujenga bwawa la kunyweshea mifugo alipofanya ziara katika Kijiji cha Msomera, Wilayani Handeni, Mkoani Tanga Aprili 11, 2022. Katika kijiji hicho kumetengwa eneo kwa ajili ya wafugaji kutoka Wilayani Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari yao ili kuendeleza shughuli zao za ufugaji.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe(kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(kushoto) walipokutana katika ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya Aprili 11, 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...