Na Muhidin Amri, Mtwara
WAKAZI 2,470 wa vijiji vya Njumbuli na Namanjele Halmashauri ya wilaya Mtwara mkoani Mtwara wameondokana na kero ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama baada ya Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma, Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike alisema kati ya wanufaika wa mradi,wakazi 1,988 wanatoka kijiji cha Njumbuli na 1,382 wa kijiji cha Namanjele.
Alisema, katika bajeti ya mwaka 2021 Serikali kupitia wizara ya maji imeipatia Ruwasa wilaya ya Mtwara jumla ya Sh. 366,940,095.38 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao umemaliza kabisa changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo.
Alisema mradi wa maji Njumbuli- Namanjele ambao umekamilika kwa asilimia 100, ulianza kujengwa mwezi April 2021 na kukamilika Mwezi Disemba chini ya usimamizi wa wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Mtwara.
Alisema,mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kusogeza na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mtwara.
Kwa mujibu wake,mradi umehusisha ujenzi wa matenki matatu yenye ujazo wa lita 50,000 kila moja,matenki mawili yamejengwa kijiji cha Namanjele na moja limejengwa kijiji cha Njumbuli,ujenzi wa virura(vituo) 11,ufungaji pampu mbili na ulazaji bomba za maji umbali wa km 11.
Alisema, katika utekelezaji wa mradi Serikali kuu imetoa jumla ya Sh.366,940,095 na wananchi wamechangia Sh.2,500,000 na kufanya fedha zilizotumika kutekeleza mradi kufikia Sh.369,440,095.
Alisema,utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na kukabidhiwa kwa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO)tangu mwezi Februari mwaka huu kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi.
Aidha alieleza kuwa,mradi umezingitia sera ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani na umezingitia umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo kimoja cha kuchotea maji kwenda kingine ambapo hadi sasa kaya 15 zimeunganishiwa maji ili kurahisisha uwepo wa maji karibu.
Mashindike alitaja faida za mradi ni kuongeza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 55.9 ya mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2022,kutatua changamoto ya maji iliyokuwepo katika vijiji hivyo.
Pia alitaja faida nyingine ni kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko katika jamii kutokana na matumizi ya maji yasio safi na salama na kuchochea maendeleo ya watu na ustawi wa Taifa.
Mashindike,ameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge Sahil Geraruma,ameipongeza Ruwasa kwa kutekeza mradi huo kwa viwango na umeandana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Hata hivyo,ameshauri kuongezwa vituo vya kuchotea maji kutoka 11 vya sasa ili kila mwananchi aweze kupata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yake,jambo litakalo saidia jamii kuona mradi huo ni wao na itakuwa rahisi kuulinda na kuchangia gharama za uendeshaji wake.
Aidha,amewashukuru wananchi waliotoa ardhi yao bure kwa ajili ya ujenzi wa miradi huo,ambapo ameiagiza Ruwasa kuwaunganishia huduma ya maji wananchi hao bila gharama yoyote.
Amewataka wananchi wa Njumbuli na Namanjele, kutunza mradi na miundombinu ambayo imetumia fedha nyingi za Serikali ambazo zingeweza kupelekwa kwa wananchi wa maeneo mengine wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii.
“Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan amewapenda sana ndiyo maana amewaleta fedha za kujenga mradi huu,sote ni mashahidi kila siku tunamuona namna anavyoangaika kutafuta fedha kwa ajili ya kusogeza na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wake,hivyo nawaomba sana muulinde mradi huu”alisema.
Amewataka wataalam(Wahandisi) wa maji kuwa na tabia ya kutembelea na kukagua miradi inayojengwa mara kwa mara ili kupata miradi yenye ubora ,badala ya kuwaacha mafundi wadogo wanafanya kazi bila usimamizi wao ili kuepusha miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma akifungua koki katika kituo kimojawapo kati ya vituo 11 vya kuchotea maji vilivyojengwa na Ruwasa kupitia mradi mkubwa wa maji wa Namanjele-Mbunjuli katika Halmashauri ya wilaya Mtwara.
Mkazi wa kijiji cha Njumbuli Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara Zaitun Mohamed kushoto,akitwishwa ndoo ya maji na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma mara baada ya kiongozi huo kufungua mradi wa maji katika kijiji hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...