Na Mbaraka Kambona, Dodoma

Wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameandaa miradi miwili (2) ya kutafiti njia mbadala ya kutibu kuku ili kudhibiti magonjwa na kupunguza matumizi ya madawa hususan ya antibiotiki yasiyokuwa ya lazima.

Hayo yalifahamika mapema leo Aprili 5, 2022 wakati timu ya wataalam kutoka SUA na Shirika la Kimataifa la Denmark la ICARS, linaloshughulika na afya za wanyama na binadamu, walipokutana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kumueleza namna miradi hiyo itakavyotekelezwa hapa nchini.

Mtafiti Kiongozi wa Miradi hiyo kutoka SUA, Prof. Robinson Mdegela wakati akiwasilisha taarifa ya miradi hiyo kwa Naibu waziri huyo alisema kuwa kumekuwa na matumizi makubwa ya dawa hususan antibiotiki kwenye ufugaji wa kuku wa kisasa kama njia ya kukabiliana na magonjwa ya kuku kwa sababu ya uchanjaji hafifu na kutokuzingatia njia za ufugaji bora hali ambayo imepelekea uwepo wa mabaki mengi ya dawa kwenye nyama na mayai ya kuku.

“Madhara ya ulaji wa mazao ya kuku yenye mabaki ya dawa ni pamoja na usugu wa vimelea kwenye dawa huku pia mfugaji akitumia gharama kubwa ya kununua dawa ambayo angeweza kuiepuka”,alisema Prof. Mdegela

Aliongeza kwa kusema kuwa kufuatia uwepo wa changamoto hiyo wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameandika maandiko mawili (2) ya miradi ya kutafiti juu ya uwezekanao wa kutumia njia za usafi kwenye mabanda ya kuku na kuchanja kuku ili kudhibiti magonjwa ya kuku na kupunguza matumizi ya madawa hizo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema miradi hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika jitihada za kuhamasisha ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wenye tija utakaohakikisha usalama wa chakula hapa nchini.

“Nawapongeza Wataalam kwa kuja na miradi hii ambayo inakwenda kutafuta suluhisho la changamoto za matumizi makubwa ya dawa kwa kuku, naomba mkasimamie vyema utekelezaji wa miradi hii ili matokeo yakaonekane kwa haraka na wananchi wawe na uhakika na chakula wanachokitumia”, alisema Mhe. Ulega

Aidha, Mhe. Ulega alilishukuru shirika la Kimataifa la ICARS la Denmark kwa kukubali kufadhali miradi hiyo miwili kwa miaka mitatu (3) kuanzia Mwezi Mei 2022 mpaka Mei 2025 huku akisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za matumizi hayo ya dawa kwa walaji lakini pia itawapunguzia mzigo wa gharama wafugaji wengi wa kuku hapa nchini.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Shirika la ICARS, Helle Engslund Krarup aliishukuru serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kwa kuruhusu miradi hiyo kutekelezwa hapa nchini huku akisema kuwa watahakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa mafanikio.

“Tunaimani ushirikiano huu utafanikiwa na miradi hii itasaidia jamii kubadili namna ya ufugaji wao na pia itasaidia taifa kuona kama kuna haja ya kutunga sera na miongozo ya ufugaji bora wa kisasa”, alisema Krarup

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akisalimiana na Mtafiti Kiongozi wa Miradi hiyo kutoka SUA, Prof. Robinson Mdegela muda mfupi baada ya timu ya wataalam kutoka SUA na Shirika la Kimataifa la Denmark la ICARS, linaloshughulika na afya za wanyama na binadamu, walipokutana Aprili 5, 2022 na Naibu Waziri huyo ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo kumueleza namna miradi hiyo itakavyotekelezwa hapa nchini.

 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Shirika la ICARS, Helle Engslund Krarup kuhusu namna shirika hilo litakavyowezesha miradi hiyo ya kupunguza matumizi ya dawa kwa kuku katika kikao kifupi kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 5, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...