Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa siasa kufanya majadiliano na kutoa mapendekezo ambayo yataleta maridhiano, haki na amani hapa nchini.
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akifungua Mkutano wa kitaifa wa haki, amani na maridhiano uliofanyika katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyama bya siasa kufanya majadiliano kwa kuzingatia hali ya siasa, uchumi na mazingira halisi ya nchi kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Rais Samia pia amesema Tanzania ilichagua mfumo wa vyama vingi ili kuiwezesha kupata maendeleo kwa haraka hivyo, amewahakikishia kuwa Serikali itashirikiana na vyama vya siasa hususan katika masuala ya kisera na kisheria ili kuijenga nchi.
Vile vile, Rais Samia amekiagiza Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Kuangalia mfumo wa wajumbe wanaounda Taasisi hiyo ili kujumuisha wawakilishi kutoka ngazi zote za kisiasa na kuhakikisha wanafikia malengo yanayokusudiwa.
TCD ni Taasisi isiyo ya Kiserikali iliyoundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mabaraza la Madiwani iliyosajiliwa mwaka 2005.
ZuhuraYunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...