
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kwa kiasi kikubwa fedha ya Watanzania imetumika kuzalisha Filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo kwa sasa inazinduliwa nchini katika mkoa wa Arusha, visiwani Zanzibar na mjini Dar es Salaam baada ya kuzinduliwa nchini Marekani.
Akizungumza katika uzinduzi wa Filamu hiyo, mjini Arusha, Rais Samia amesema Watanzania wote wamefanikisha kupatikana kwa Filamu hiyo ambayo itaitangaza nchi, duniani kwa kuwa na vivutio mbalimbali vya Utalii.
“Uzinduzi wa kule Newyork Marekani sikuona uzuri wa picha, nilikuwa na woga kweli kweli kwamba Watanzania wataipokeaje, inatokaje, ikoje, ni kitu gani hicho? Lakini baada ya uzinduzi tu, tulianza kupata salamu zaidi ya watu laki 3 na zaidi kutoka Ulimwenguni wanaipongeza hii Filamu”, amesema Rais Samia.
“Hata kule Los Angeles tumeiona pia, na tumepata mrejesho mzuri tu, na hapo nimepata imani kuwa tulichokifanya basi ni kitu kizuri na kizuri kwa nchi yetu”, ameeleza Mhe. Rais
Aidha, Mhe. Rais ameeleza kuwa kutumia siku nane nje ya Ofisi, kufanya Filamu hiyo, baadhi ya Vijana wa Kitanzania walimbeza kushiriki kwake katika Filamu hiyo, amesema kutokukaa Ofisini siku nane na kutohudumia Wananchi siku hizo, italipa zaidi, kwa kuwa na Filamu inayoitangaza nchi Kimataifa.
“Kuna Wadogo zangu, Wanangu nilikuwa nasoma kwenye Mitandao ya Kijamii, wanasema huyu Mama baada ya kufanya kazi, kajigeuza ‘Rambo’, amejigeuza ‘Schwarzenegger’ anafanya Filamu! Lakini nikasema ngoja tuone kitakachotoka.” Ameeleza.
Pia, Rais Samia amesema baada ya kuonekana Filamu hiyo nchini Marekani, idadi kubwa ya watu ulimwenguni wameahidi kuja nchini Tanzania kutokana na kuvutiwa na vivutio vya Utalii nchini na hatimaye Taifa kupata Fedha za kigeni, Kodi, na Vijana wengi kupata ajira kupitia Sekta ya Utalii.
Kwa upande wake, Muandaaji na Mzalishaji wa Filamu hiyo ya ‘Royal Tour’ Peter Greenberg na mwenzako John wamesifu uhusika wa Rais Samia katika kupata maudhui ya Filamu hiyo, huku wakisifu utajiri wa Rasilimali mbalimbali za Taifa la Tanzania, ikiwemo Utamaduni wa Makabila mbalimbali, tunu ya Wanyama mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...