*Ahaidi kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani, umoja na ushirikiano

ASKOFU Rose Mgeta amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa makanisa ya Mountain of Fire Church Tanzania (Mlima wa Moto,) akichukua nafasi ya  Hayati ya Mama Getrude Rwakatare aliyefariki dunia Aprili 20, 2020.

Akizungumza mara baada ya kuwekwa wakfu na  kusimikwa rasmi Askofu Rose Mgeta amesema, amekaimu nafasi hiyo kwa takribani miaka miwili hivyo anaamini ataendeleza alipoishia Hayati Mama Rwakatare kwa kuwaunganisha waumini katika misingi ya imani, upendo, umoja na ushirikiano.

Askofu Mgeta amesema, kwa kushirikiana na viongozi wa dini watashirikiana na Serikali katika kudumisha amani na utulivu kwa kuhubiri kwa waumini ili kulinda tunu ya utulivu wa Taifa la Tanzania.

"Tupo pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan katika kulinda tunu za taifa, tutahubiri amani kwa waumini ili kuzidi kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja." Amesema.

Kuhusiana na wanawake kushika nafasi za juu za uongozi Askofu Mgeta amesema kuwa, wanawake wanaweza kutendea kazi nyadhifa wanazoshika na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

"Wanawake tunaweza, nimekaa na kujifunza kupitia mwanamke mpambanaji Hayati Mama Rwakatare na tunafahamu mchango wake katika sekta muhimu .......na sasa tunaona jitihada za Mama Samia katika ujenzi wa Taifa, nitayaenzi na kuyaendeleza aliyoanzisha Hayati Mama Rwakatare hasa katika kuwainua wanawake kwa nguvu zaidi." Amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa shule za St. Mary's Dkt. Rose Rwakatare amesema, utendaji kazi wa Askofu Mgeta utawaleta waumini pamoja katika kujenga Taifa.

"Wanawake tunaweza kufanya makubwa na tunaamini Mama Mgeta atavaa viatu vya Hayati Mama Rwakatare kwa kuwa ametumikia hapa kwa muda mrefu....Kanisa na Maaskofu tutazidi kuombea amani na utulivu wa Taifa letu." Amesema.

Askofu Mgeta mwenye shahada ya Theolojia na masuala ya uongozi na utawala ameelezwa kuwa na huruma, mwadilifu, mchapa kazi na mwenye maono na kazi ya Mungu pia anaaminiwa kuliongoza kanisa hilo kwa weledi.


Askofu Mkuu wa Makanisa ya Mountain of Fire Church - Tanzania (Mlima wa Moto,) Rose Mgeta akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa Makanisa hayo na kuahidi ushirikiano katika kuliendeleza Kanisa hilo, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa shule za St. Mary's Dkt. Rose Rwakatare akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mkuu Rose Mgeta na kueleza kuwa wana imani kubwa na Askofu Mgeta hasa katika kuliongoza kanisa hilo leo jijini Dar es Salaam.



Matukio mbalimbali katika picha wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu Rose Mgeta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...