Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC rasmi wamefuzu Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) msimu wa 2021-2022 baada ya kupata ushindi wa bao 4-0 dhidi ya USGN ya Niger katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba SC wamefuzu Robo Fainali ya Michuano hiyo baada ya kuangukia nafasi ya pili ya Kundi D lililokuwa linaudwa na timu za RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na USGN ya Niger. Mnyama ameangukia nafasi ya pili kwa kukusanya alama 10 sambamba na vinara wa Kundi hilo, RS Berkane wenye alama 10 ambao wamepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Asec Mimosas.
Katika mchezo wa mwisho uliohitimishwa majira ya Saa 6 Usiku, kwa Saa za Afrika Mashariki, Simba SC ilijihakikishia ushindi huo katika Kipindi cha pili cha mchezo, baada ya Kipindi cha kwanza kutoka sare ya 0-0 licha ya shinikizo kubwa la Wachezaji wa Simba SC katika lango la USGN.
Mabao ya Simba SC yalifungwa na Kiungo Sadio Kanoute dakika ya 63 ya mchezo baada ya kupiga Shuti kali lililomshinda Golikipa wa USGN, Saidu Hamisu. Bao la pili likiwekwa wavuni na Mshambuliaji Chris Kope Mugalu dakika ya 68, akifunga pia bao la tatu katika dakika ya 78, bao la nne, USGN walijifunga baada ya Golikipa kujichanganya dakika ya 84.
Baada ya kufuzu hatua hiyo, Simba itajizolea kitita cha Dola za Marekani 350,000 (sawa na zaidi ya Milioni 800 za Kitanzania) huku wakisubiri kupangwa na timu ambayo watacheza nayo hatua ya Robo Fainali katika Michuano hiyo

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...