Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa wananchi hapa visiwani, wameelemewa na viwango tofauti vya ugumu thakili wa maisha, licha ya ulimwengu mzima sasa kukabiliwa na hali hiyo.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, katika Kijiji cha Tumbe-Rahaleo, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, akisalimiana na viongozi na wananchi mbali mbali, waliojitokeza kumpokea, akiwa katika Ziara yake Maalum ya Siku Nne, kisiwani hapa.
Hiyo ni sehemu pia ya salamu za Mheshimiwa Othman, akikamilisha Ziara yake katika Mikoa yote Mitano na takriban Majimbo 50 ya Unguja na Pemba, alipowatembelea na kuwajulia hali, pamoja na kujumuika nao katika Iftari, wananchi mbali mbali wanyonge na wahitaji wakiwemo wajane, yatima na wazee wasiojiweza, tangu mwanzoni kabisa mwa mwezi huu.
Amesema kuwa, kubaini viwango vya hali duni ya maisha magumu yanayowasibu wananchi waliowengi, ni vyema kuwafikia, kuwatembelea ana kwa ana, na hatimaye ikibidi kuwafikiria kwa kuwatafutia namna bora ya kuwasaidia kwa hali na mali, ili kuwawekea mazingira angalau ya kujikimu katika Misimu hii ya Kheri, hasa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Ndugu zangu uzito wa ugumu wa maisha ni wa viwango tofauti mathalan ujazo wa kilo tano na wengine kilo kumi na zaidi kwa kuendelea”, amesisitiza Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo–Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba, Bw. Hamad Omar Bakar ‘Small’, ameeleza hali ya faraja na matumaini mema waliyokuwa nayo wananchi, hasa pale walipomuona Mheshimiwa Othman na Viongozi wengine, wakikata mitaa, ‘jua-mvua’ ili kuwafikia wanyonge, hata iwapo mazingira yalikuwa magumu kupita kiasi.
Katika ziara yake hiyo, Mheshimiwa Othman alijumuika na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, Masheha wa baadhi ya Shehia, Vyama vya Siasa, na Vikosi vya Ulinzi na Usalama wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba.




(Picha na Kitengo cha Habari Ofisi ya makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...