Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam,Meneja Habari na Uhusiano Shirika la Nyumba la Taifa,Muungano Saguya amesema shirika hilo limepanga kutekeleza miradi yake mbalimbali, lengo likiwa ni kukuza mapato ili kuweza kuwahudumia Watanzania.
Amesema Vipaumbele ambavyo uongozi mpya wa Shirika hilo unaenda kuvizingatia ni pamoja na kukamilisha miradi mikubwa iliyosimama ya Morocco Square na Kawe 711jijini Dar es Salaam ambayo ilisimama tangu mwaka 2018 kutokana na upungufu wa fedha.
" Shirika limepewa kibali cha awali na Serikali ya Awamu ya Sita cha kukopa shilingi Bilioni 173.9 kumalizia miradi hiyo. Tayari Hazina imeshaidhinisha mkopo wa Shilingi Bilioni 44.7 na tayari utekelezaji wa miradi hii unaendelea'',amesema Saguya .
Amesema sambamba na mpango wa awali wa biashara (Business Plan) wa eneo la Kawe, Shirika limeandaa mpango wa kujenga nyumba 360 za makazi ya watu wa kipato cha kati na maduka ya biashara (Shopping Malls) katika eneo hilo la Kawe.
''Katika kusaidia suala la makazi hasa baada ya Serikali kuhamia Dodoma, Shirika litaendelea kujenga nyumba katika jiji la Dodoma, ambapo ujenzi utakaofanyika ni pamoja na nyumba za makazi za Medeli awamu ya III, Iyumbu awamu ya III (Nyumba za ghorofa) na miradi mingine baada ya kupata ardhi ya uendelezaji'',amesema Saguya.
Saguya amefafanua pia kuwa Shirika litaendelea kujenga nyumba za kuuza na kupangisha katika maeneo mbalimbali ya mikoa kwa kutumia ardhi itakayopatikana au kwa kutumia ardhi nafuu.
" Katika hili Shirika pia litaimarisha maeneo ya mipaka yetu kwa kujenga majengo makubwa ya biashara kama ilivyofanyika katika eneo la Mutukula, mpaka wa Tanzania na Uganda",amesema
Saguya ameeleza kuwa Kuendelea kukamilisha ujenzi wa majengo 8 ya Wizara mbalimbali za Serikali katika mji wa Mtumba Jijini Dodoma (awamu ya pili). Miradi hii itakapokamilika itagharimu jumla ya TZS Bilioni 186.83. Msisitizo umewekwa katika kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati kwa kuongeza usimamizi, udhibiti na ubora wa majengo hayo,"
Amesema NHC itaendelea kukaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili kufanya uendelezaji wa majengo ya biashara na makazi katika maeneo na viwanja vya Shirika vilivyo wazi hivi sasa.
"Hii inakusudia kusaidia kuongeza mapato ya Shirika, mapato ya Serikali, kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania. Mpango wa kushirikisha sekta binafsi umeshaandaliwa na utawekwa wazi kwa umma muda mfupi ujao na utazingatia vigezo na masharti yenye tija kwa Shirika, wawekezaji na Taifa",amesema Saguya.
Akifafanua kuhusu ukusanyajii wa Madeni,Saguya amesema wameendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia shilingi bilioni 22 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia shilingi bilioni 11.1. Msisitizo ukiwa ni kuhakikisha kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha Shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali hizi za umma.
" Tutaendelea kushirikiana na Taasisi na wadau mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi yetu hususan ushiriki wao wa kuweka miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya ujenzi'',amesema Saguya.
Amesema Shirika litaendelea kusimamia miliki ya nyumba zake zipatazo 18,622, kwa kuzifanyia matengenezo ipasavyo kupitia Mpango wa Matengenezo ya nyumba wa miaka mitano (2021/22-25/26). Katika kufanikisha hilo Shirika limetenga shilingi Bilioni 50 kutekeleza mpango huo,amesema na kuongeza kuwa huo ni ukarabati mkubwa utakaohusisha kubadilisha paa, vyoo na madirisha chakavu,"



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...