Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Jenista amesema, upo umuhimu mkubwa wa kufanya ukaguzi kwenye taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi kama za afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.

Akizitaja faida za ukaguzi wa rasilimaliwatu, Waziri Jenista amesema, una faida kubwa kwa Serikali, Waajiri, Watumishi wa Umma na Watanzania kwa ujumla ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake.

Ameongoza kuwa, unazisaidia pia taasisi zilizokaguliwa kurekebisha kasoro za kiutendaji ambazo zimebainishwa wakati wa ukaguzi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia amesema ukaguzi huo unaiwezesha Serikali kufahamu hali ya utendaji kazi iliyopo katika taasisi za umma na kuziwezesha mamlaka husika kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa taasisi zote za umma.

Sanjali na hayo, Waziri Jenista amesema ukaguzi huo unaipa fursa Tume ya Utumishi wa Umma kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya namna bora ya kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili iwe na tija kwa umma na taifa kwa ujumla.

Kuhusiana na migogoro ya kiutendaji inayojitokeza kwenye baadhi ya taasisi, Mhe. Jenista amesema taasisi hizo zikitekeleza maelekezo ya Tume baada ya kufanyiwa ukaguzi zitaepusha migogoro kwa kiasi kikubwa.

Tume ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu kwenye Taasisi za Umma 110, hivyo taarifa ya ukaguzi huo inaandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua stahiki.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...