Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kimepanga kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na uhaba wa vipimo vya kidigitali nchini kwa kuanzisha mitaala itakayowawezesha wanafunzi kuanzisha kampuni za kutengeneza vipimo hivyo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema, wakati wa maadhimisho ya siku ya vipimo duniani yaliyofanyika chuoni hapo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘vipimo katika ulimwengu wa kidigitali’
Profesa Mjema alisema elimu ya juu inapaswa kutatua changamoto za nchi badala ya wahitimu wake wengi kutegemea kuajiriwa hivyo wanafunzi lazima waandaliwe kutengeneza fursa za ajira kwa wenzao.
Aidha, Profesa Mjema alisema kwa nchi zote za Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi pekee inayofundisha kozi ya vipimo na mizani kupitia chuo cha CBE lengo ikiwa ni kutatua uhaba wa wataalamu wa fani hiyo kwenda ukanda huo.
“Kauli mbiu ya mwaka huu imechaguliwa kwasababu teknolojia hii ya kidijitali inatumika maeneo mengi duniani kwa mfano matumizi ya akili bandia artificial intelligence, inatumika sana kwenye masuala ya vipimo duniani,” alisema Profesa Mjema
Aidha, alisema hata Tanzania vipimo vingi vinavyotumika kwa sasa ni vya kidijitali akitoa mfano wa mizani inayotumika kwenye maduka mengi ya kuuzia nyama na vipimo vya kupita joto la mwili wa binadamu kwenye hospitali mbalimbali.
“Wengi mtakumbuka zamani kupimwa joto unawekewa kile kipimajoto mdomoni sasa kwa mazingira ya sasa magonjwa yalivyo mengi hebu fikiria kama bado tungekuwa tunatumia kipimo hicho nani angekubali kuwekewa lile lidude mdomoni mwake likiwa limetoka kwenye mdomo mwingine,” alihoji
Alisema hata vipimo vya ujazo wa mafuta kwenye matenki umebadilika kwani badala ya utaratibu wa zamani wa kupanda juu ya gari na kuingiza fimbo ndani ya tenki la mafuta sasa mtu anaweza kujua ujazo wa mafuta akiwa nje .
“Ulimwengu wa kidijitali umeleta mapinduzi makubwa sana naamini hata chuo cha elimu ya biashara kwa kuwa ndicho kinaongoza kwenye kozi hii ya vipimo lazima twende kidijitali isiwe ulimwengu unaenda kule sisi tunabaki kizamani,” alisema
Alisema elimu ya kidijitali itakuwa na msaada mkubwa kwa jamii ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata vipimo sahihi wanapokwenda kununua bidhaa mbalimbali.
“Vipimo vya kizamani wananchi waliibiwa sana, yale mawe yalikuwa yanakwanguliwa mpaka yanapoteza uzito flani. Mwuzaji anakuwa na mawe feki na halisi akija mtu anaonekana onekana kwamba hajui mambo anabambikiwa jiwe feki lakini akija anayeonekana mjanja mjanja anawekewa jiwe sahihi lakini kwa dijitali haya yote hayapo tena,” alisema
Mkuu wa Chuo cha Elimu Biashara (CBE), Prof Emanuel Mjema, (katikati) akiongea na wanafunzi wakati wa maadhimisho ya siku ya vipimo duniani, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wa pili kulia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof Edda Lwoga.
Mkuu wa Chuo cha Elimu Biashara (CBE), Profesa Emanuel Mjema akiangalia maonyesho ya vipimo wakati wa maadhimisho ya siku ya vipimo duniani, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam chuoni hapo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...