Na Mbaraka Kambona, Uvinza

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanatengeneza miundombinu mizuri na kuwapatia Wavuvi wanaoishi kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na maeneo mengine  vifaa vya kisasa vya uvuvi ili viwasaidie  kuongeza thamani ya zao la Dagaa  na kupunguza upotevu wa zao hilo baada ya kuvua.

Ulega aliyasema hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika vijiji vya Buhingu na Katumbi vilivyopo wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 6 - 7, 2022.

Wakati akiongea na Wavuvi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kukuza uchumi wa buluu na ndio maana inatengeneza miundo mbinu mizuri ya kuchakata dagaa na mazao mengine ya samaki ili kuwaongezea thamani na waweze kuuzika kwa bei nzuri  na wananchi wafaidike na zao hilo.

"Tunataka tuone zao la dagaa ambalo huku kigoma linazalishwa kwa wingi linainua maisha ya watu, hatutaki kuona hata dagaa mmoja anapotea kwa kuharibika au kuoza, lengo letu ni kuona ukanda wote huu wa Ziwa Tanganyika mnanufaika ipasavyo kupitia dagaa", alisema

Aliongeza kuwa  wanawapatia Wavuvi hao vifaa ikiwemo Boti, injini, nyavu, kamba na taa lengo likiwa ni kufanya Uvuvi endelevu na kulifanya zao la Dagaa kuwa la kimkakati ili liwe chachu ya maendeleo kwa wavuvi hapa nchini.

"Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo tunaendelea kutengeneza miundombinu mizuri ya kuchakata dagaa na mazao mengine ya samaki katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao hayo na kuyaongezea thamani ili yauzwe kwa bei nzuri ndani na nje ya nchi", alifafanua

Aidha, aliwataka wananchi wanaoishi kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika kuendelea kutunza na kuhifadhi mazalia ya samaki ili uvuvi katika eneo hilo uwe endelevu  kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Hanaf Msabaha alisema kuwa kuna haja Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki Wilayani humo ili samaki waweze kupatikana muda wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane ambao unatekelezwa Mkoani Kigoma, Bw. Lukindo Hiza alisema tayari wameshirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Uvinza kwa ajili ya kujenga Mwalo wa kisasa  utakaosaidia kupunguza upotevu wa dagaa na  wataweza  kuwaongezea thamani ili wawauze kwa bei nzuri zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Pichani ni sehemu ya vifaa vilivyokabidhiwa kwa Wavuvi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega katika  tukio la makabidhiano lililofanyika katika Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 7, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wavuvi wa Kijiji cha Buhingu kilichopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 7, 2022 alipofanya ziara katika Kijiji hicho ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya miaka 10 ya Mradi wa Tuungane yaliyofanyika Mkoani Kigoma Mei 5, 2022. Mradi huo wa Tuungane ambao unatekelezwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika umejikita katika kutunza mazalia ya Samaki, kupunguza Uvuvi haramu na kuwezesha wachakataji wa mazao ya Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua taa za kufanyia uvuvi wa dagaa kabla ya kukabidhi vifaa vya kuvulia dagaa kwa wavuvi   katika Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 7, 2022. Vifaa alivyokabidhi Mhe. Ulega kwa wavuvi vilitolewa na Mradi wa Tuungane  ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya miaka 10 ya Mradi huo yaliyofanyika Mkoani Kigoma Mei 5, 2022. Mradi huo wa Tuungane ambao unatekelezwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika umejikita katika kutunza mazalia ya Samaki, kupunguza Uvuvi haramu na kuwezesha wachakataji wa mazao ya Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akipatiwa maelezo na Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane, Bw. Lukindo Hiza (wa tatu kutoka kulia) kabla ya kukabidhi vifaa vya kuvulia dagaa kwa wavuvi wa Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma Mei 7, 2022.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...