Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Lindi

BAADA ya ukimya wa muda mrefu hatimaye aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano katika serikali ya Awamu ya Nne Barenard Membe ametoa sababu kuu mbili zilizomfanya arejee tena kwenye Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Membe alivuliwa uanachama wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano , hivyo aliamua kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo na kisha kupata nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama hicho lakini baadae alijiondoa kabla ya CCM kumrejesha.

Mwanasiasa huyo mbobezi wa diplomasia ya kimataifa leo Mei 29,2022 kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Lindi, Membe amesema amerejea CCM akiwa na sababu mbili za msingi.

Akitoa sababu hizo mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka, Mbunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye, viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali pamoja na wananchi Membe amefafanua kati ya Machi 30 hadi Aprili 1 ,2022 aliitwa Dodoma kwenye Mkutano wa Kamati Kuu ya Maadili na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu ambapo alipata nafasi ya kuzungumza.

 “Mama yetu ,Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa  CCM Taifa alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa na wajumbe wa Halmashauri Kuu.Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM.

“Nimerejea CCM kwa sababu kuu  mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu na wote wakinitaka nirejee CCM.

 “Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,”amesema Membe wakati akitangaza kwake kurejea tena kwenye Chama hicho na kukabidhiwa kadi ya uanachama na Shaka.

Membe amesema sababu ya pili imetokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini.“Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisonekana sana, na ninyi wananchi mlisikitika, mlisononekana.

“Sababu zote zilizonifanya niondoke CCM sasa haziko tena, narudi tena sababu zilizoniondoa CCM haziko tena.Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu  kunirudisha.Nimerudi kwenye Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, chama kilichonisomesha.”

Ameongeza “Naahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu.Kurudi kwangu CCM nieleze tu nitaendelea kukitumikia Chama changu na nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu kuleta maendeleo.

“Mwaka 2015 wakati naachia nafasi ya ubunge kwenye jimbo letu (Mtama) nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Nape pamoja na mimi mbunge wa chini chini.”

Kwa upande wake Mbunge wa Mtama ambaye pia ni Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema amefurahi Membe kurejea CCM na leo amekabidhiwa kadi ya uanachama.

“Leo Mwenyezi Mungu ameturudishia faraja wananchi wa Rondo,ameturejeshea furaha Chiponda. Mtama ni wastaarabu na hatuna shida tena , tuna imani kubwa na Membe , alinikabidhi kijiti na kuvaa viatu vyake, kulikuwa na mambo yaliyokwama huki nyuma kwasababu za kisiasa lakini Mama Samia amekuja ameziondoa,”amesema.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mtama kushikamana , fitina ambazo ziliingia kati zimekwisha.“Membe amenipigania kwenye mambo mengi, nilipotaka ubunge jimbo la Ubungo baada ya kuona kuna fitna zimeingia aliamua kuchora ramani.

“Ndio maana safari yangu ya ubunge jimbo la Mtama ilikuwa nyepesi.Kaka Membe amenipigania sana na bahati nzuri amerudi CCM.Niseme tu Mungu ameamua ugomvi.”amesema.

Wakati huo huo Shaka aliyekuwa mgeni rasmi kwenye tukio hilo la Membe kukabidhiwa kadi ya uanachama wa CCM, ameeleza  Membe amerejeshwa kwenye Chama baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake kisha na vikao vya juu.

“Membe ni miongoni mwa wanachama wengine zaidi ya 1670 waliovuliwa uanachama ambao wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, sasa wanaweza kukabidhiwa kadi zao katika matawi yao.

“Kurejea kwa Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususan kwa wanaccm wa Jimbo la Mtama,”Amesema Shaka huku akitumia nafasi hiyo kuelezea kwa kina hatua zinazochuliwa na Rais Samia katika kuleta maendeleo ya wananchi.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka HAMDU Shaka akimkabidhi ya CCM,aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyerejea CCM, katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe anayebusu kadi ya CCM baada ya kukabidhiwa na Shaka katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka HAMDU Shaka akimkaribisha CCM, aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyerejea CCM, wakati wa Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akipokipokea Kadi za Wanachama zaid ya 1600 Walio rejesha kadi za Vyama Vya Upinzani katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...