Na Mashaka Mhando, Tanga


UWEKEZAJI mkubwa uliofanywa na serikali katika bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha maji, utaisaidia kuongeza mapato na kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea bandari hiyo jana, wadau wanaohudhuria mkutano unaojadili changamoto zinazoikumba bandari ya Dar es salaam, walisema upanuzi wa gati katika bandari ya Tanga utasababisha waweze kuhudumia meli kubwa.

Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Wakala wa Meli nchini (TASAA) Daniel Malango alisema mabadiliko yaliyofanyika yanaleta suluhisho la meli zilizokuwa zikishushia mizigo nchi jirani ya Kenya, zitafika katika bandari hiyo.

"Tulichokiona Tanga tunaweza kusema ni 'game changer' kwamba kuna uwekezaji serikali imefanya, sasa naiona Tanga inakuwa suluhisho la mizigo iliyokuwa inapitia bandari ya Mombasa, Meli kubwa zitafika hapa na Revenue zetu zitakuwa juu," alisema Malango.

Alisema matayarisho yaliyofanywa kwa ajili ya kontena na mizigo mingine itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa mapato yatapanda, lakini pia wasafirishaji watatumia muda mfupi zaidi.

Naye Ofisa Sera, Mazingira wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) Anna Kimaro alisema maboresho yaliyofanywa na serikali yataleta fursa kwa wadau wanaosafirisha mizigo kwenda nchi mbalimbali kuwa na chaguo lingine la bandari.

Alisema pia itaisaidia kupunguza msongamano na mlundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam na hivyo kuisaidia serikali kupata mapato, lakini pia kusaidia mikakati ya serikali kuhudumia mizigo katika nchi jirani za Maziwa Makuu.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka alisema mradi wa maboresho ya bandari katika kuhudumia mizigo kutoka tani laki saba hadi kufikia tani milioni tatu unaofanywa katika bandari hiyo utasaidia kufikia kina cha mita 13 utasaidia meli kubwa kuweka gati bandarini.

Alisema mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza mizigo inayohudumiwa katika bandari ya Dar es salaam hasa kwa wakazi wa mikoa ya Kaskazini na kwasasa watatumia muda mfupi kupitia bandari ya Tanga.

Awali meneja wa bandari ya Tanga, mhandisi Masoud Mrisha alisema mradi huo ambao upo awamu ya pili ya utekelezwaji wake umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kukabidhiwa Novemba mwaka huu utakaokuwa na mita 450.

Alisema mradi huo ukikamilika utaweza kuhudumia kiasi cha tani milioni 3 ambapo kwa sasa bandari hiyo inauwezo wa kuhudumia shehena ya tani laki saba tu.


Meneja wa Bandari ya Tanga Mhandisi Masoud Mrisha akizunguma na waandishi wa HabariMakamo Mweyekiti wa Chama Cha Wakala wa Meli nchini (TISAA) Daniel Malonga
Meli inayochimba kuongeza kina cha maji katika bandari ya Tanga
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...