Jumla ya vijana 5,700 wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ufundi Stadi kwenye fani za Ufundi Bomba wa Viwandani, Uchomeleaji na Mekatroniki kwenye vyuo vya VETA kupitia mradi wa Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo ya Afrika(E4D) chini ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Akizungumza wakati wa hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya Utekelezaji wa Mradi wa E4D kati ya VETA na GIZ, sambamba na makabadhiano ya vifaa vya TEHAMA jijini Dodoma leo tarehe 26 Mei, 2022, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema mradi huo unaendana na mipango na mikakati ya Serikali vya kuwezesha ujuzi na ajira kwa Watanzania.

“Mradi wa E4D una mchango katika mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi.Tunapozungumzia maendeleo ya viwanda tunatambua mchango mkubwa wa VETA katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi kupitia mafunzo ya ufundi stadi hivyo mradi huu utawezesha ongezeko la vijana wenye ujuzi kwa maendeleo ya viwanda na uzalishaji ajira hapa nchini,”amesema.

Profesa Kipanyula amepongeza ushirikishwaji wa Chama cha Waajiri nchini (ATE) kwenye utekelezaji wa mradi huo ambao wana mchango mkubwa katika kutoa taarifa sahihi za mahitaji ya waajiri ili hatimaye VETA iweze kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji hayo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, ameishukuru GIZ kwa mradi huo utakaochangia katika kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya VETA nchini na kuwezesha VETA kupata vifaa vya kisasa vya kufundishia vinavyoendana na kasi ya mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia.

Amesema mafunzo yatakayotolewa kwenye mradi huo yatajikita kwenye fani za Uchomeleaji (Welding), Ufundi Bomba wa Viwandani (Industrial Plumbing) na Mekatroniki (Mechatronics) kwenye vyuo vya VETA vya Mikoa ya Dodoma, Manyara na Lindi.

Mkurugenzi Mkazi wa GIZ Tanzania, Dkt. Mike Falke, amesema mradi wa E4D unaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kukuza ujuzi na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na wanawake.

Meneja Mradi wa E4D, Ndugu Awadh Milasi, amesema utekelezaji wa mradi huo hapa nchini ulianza mwezi Juni, 2021 na unatarajiwa kumalizika mwezi Desemba, 2023.

Amesema jumla ya vijana 1,600 watakaonufaika na mradi huo watapata mafunzo kwa njia ya VSOMO (Mafunzo ya Ufundi stadi kupitia simu za mkononi) yanayoratibiwa na Chuo cha VETA Kipawa ikiwa ni kuwezesha matumizi chanya ya teknolojia.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu wa Wizara hiyo Profesa Maulilio Kipayula  akizungumza wakati wa hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya Utekelezaji wa Mradi wa E4D kati ya VETA na GIZ, sambamba na makabadhiano ya vifaa vya TEHAMA katika hafla iliyofanyika  jijini Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore akitia Saini Randama ya Ushirikiano wa Utekelezaji wa Mradi wa E4D kati ya VETA na GIZ, sambamba na makabadhiano ya vifaa vya TEHAMA katika hafla iliyofanyika  jijini Dodoma
Mkurugenzi Mkazi wa GIZ Tanzania, Dkt. Mike Falke, akitia Saini Randama ya Ushirikiano wa Utekelezaji wa Mradi wa E4D kati ya VETA na GIZ, sambamba na makabidhiano ya vifaa vya TEHAMA katika hafla iliyofanyika  jijini Dodoma
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...