Na Mwandishi wetu - Bungeni Dodoma
BAADHI
ya wabunge wameonyesha kuchukizwa na vitendo vya ukatili vinavyoendelea
hapa nchini hususan matukio ya ulawiti na ubakaji wa watoto ambapo
wametoa maoni tofauti huku baadhi yao wakitaka wanaume wanaofanya
vitendo hivyo wahasiwe ili kuwanusuru watoto dhidi ya vitendo vya
ubakaji na ulawiti.
Wakichangia
mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na
Makundi Maalum ambayo imeomba shilingi bilioni 43.403 kwa mwaka wa Fedha
wa 2022/23 bungeni jijini Dodoma,wabunge hao wamesema matukio hayo ni
miongoni mwa mambo ambayo yanaathiri malezi na makuzi ya watoto wadogo
na hivyo kuathiri makuzi katika maisha yao.
Mbunge
wa Viti Maalum Subira Mgalu amesema, takwimu za matukio ya ukatili
zinatisha huku akisema kwa kipindi cha Januari 2019 mpaka sasa matukio
hayo jumla yake ni takribani 29,000 lakini miongoni mwao kubakwa ni
takribani 19,000 sawa na asilimia 70 huku yaliyofikishwa mahakamani
yakiwa ni asilimia 75 na yaliyohukumiwa ni kama asilimia 67.
“Tatizo
hili ni kubwa na katika moja ya changamoto ni matukio ya kulawiti
ambapo watoto wa kiume zaidi ya 3000 kati ya 3,260 sawa na asilimia 64
wamelawitiwa,hali hii inatisha mpaka tunatamani kama adhabu iongezwe ,au
tuseme wanaume wahasiwe ,hii yote ni kuona namna gani tuanweza kuondoa
ukatili huu wa ulawiti na ubakaji wa watoto,
“Serikali
inafanya maendeleo kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho lakini
maendeleo haya yatakuwa hayana maana kama tunaandaa kizazi cha watoto
wanaobakwa ,watoto wa kiume wanaolawitiwa,
“Kwa
hiyo naiomba Serikali kupitia Wizara mtambuka zinazohusika katika eneo
hilo ,kuangalia sheria kwani pamoja na kwamba zipo lakini haipiti wiki
yanasikika matukio ya ubakaji,ulawiti wa watoto,
“Na
kinachosikitisha zaidi matukio yameambukiza ndani ya familia,unakuta
baba anabaka watoto wake ,baba analawiti watoto wake,tumnwombe mwenyezi
Mungu atuongoze tuondokane na haya matukio.”
Mbunge
huyo aliwaasa watanzania kutahimini kwa matukio hayo ambayo yamekuwa
yakijiotokeza kila siku huku akiiomba mahakama mahakama iendelee
kutenda haki katika kuhakikisha walawiti na wabakaji wa watoto
wanachukuliwa hatua stahiki.
Kwa
upande wake Mbunge wa Viti Maalum Fatma Toufiq (CCM) amepongeza
mikakati mbalimbali ya serikali iliyopo ambayo inalenga kuhakikisha
ukatili unatokomezwa kupitia Mpango wa Mpango Kazi wa Taifa wa
Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambao una
dhamira ya kuhakikisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto unatokomezwa
kwa asilimia 50 ifikapo Juni 2022.
Hata
hivyo amesema,kumekuwa na ukatili mwingi hapa nchini ukiwemo wa kingono
,vipigo ,kuuawa,kuchomwa moto watoto,usafirishaji watoto,ubakaji wa
watoto,ulawiti wa watoto,huku akisema,kwa matukio hayo inaonyesha
ukatili umekithiri kupita kiasi .
“Na
pia kwa kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa mbalimbali
vimekuwa vikiripoti kuwa wahusika wa matukio ya ukatili hususan wa
ubakaji wa watoto ni pamoja na ndugu wa karibu ambao ni baba ,ndugu wa
karibu wanabaka na kulawiti watoto vitendo ambavyo vina athari kubwa
katika Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya mtoto,
“Nitoe
mfano wa matukio ambayo yameripotiwa hivi karibuni Mkoa wa Kilimanjaro
kuna mume amemuua mkewe mbele ya mtoto wake wa miaka miwili,sasa huyu
mtoto akikua akili yake itakuwaje hilo ni tatizo,kuna mtoto alinyongwa
Machi mwaka huu ,kuna tukio la baba kumuua mtoto wake kwa kushindwa
kusoma ,kuna mama mkubwa naye amemuua mtoto wa mdogo wake,kwa hiyo mambo
haya yanatisha ,.”amesema Toufiq
Mbunge
huyo pia ameiasa Serikali kutupia macho shuleni huku akisema kuna
matukio ya ubakaji na ualwiti yamekuwa yakifanyika huko kwa watoto walio
katika madarasa ya juu kuwafanyia vitendo hivyo watoto wenzao wa
madarasa ya chini .
Baadhi
ya shule zetu nazo siyo salama,baadhi ya watoto wa madarasa ya juu
wamekuwa wakiwalawiti watoto wa madarasa ya chini na hili jambo nalo
inapaswa tuliangalie kwa kuona jinsi tunavyoielimisha jamii,maana
inawezekana baadhi ya tabia za watoto wanazirithi kutoka katika nyumba
na familia zao.
Kufuatia
changamoto hizo za ukatili Toufiq ameishauri Serikali kuiangalia upya
sheria ya kanuni ya adhabu kuhusu mimba zinazotokana na kubakwa na ndugu
wa damu ili iwaondolee sonona walengwa (wasichana) na kama itafaa
ujauzito utolewe na wataalam.
Ameiomba
Serikali kuchukua hatua kwa wazazi wa kiume wanaotelekeza watoto wao
kwa sababu baadhi ya akina mama wanashindwa kuwalea watoto na hivyo
kuathiri Malezi na makuzi yao na hatimaye kushindwa kukua hadi kufikia
utimilifu wao.
Awali
Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum
Dkt.Dorothy Gwajima alisema, pamoja na hatua za kila siku za Serikali na
wadau mbalimbali kupambana na ukatili
kupitia
MTAKUWWA, Wizara inaratibu utekelezaji wa kampeni kubwa ya kupambana na
ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya kubaini viashiria vya ukatili
na kuchukua hatua za kuzuia.
Aidha
alisema,kwa kuwa utekelezaji wa MTAKUWWA unafikia ukomo mwezi Juni
mwaka huu, Wizara imeanza mchakato wa kufanya tathmini ya Mpango huo kwa
lengo la kubaini mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji kwa
kipindi cha miaka mitano, changamoto na upungufu wa kimuundo na
kiutendaji ulioathiri kufikiwa kwa malengo ya Mpango.
“Tathimini inatarajiwa kubainisha masuala ya kuigwa na kutoa mapendekezo ya namna bora zaidi ya kukabiliana na changamoto
na
upungufu uliobainika,matokeo au mapendekezo yatakayobainishwa katika
taarifa ya Tathmini ya Mpango yatawezesha kuanza kwa maandalizi ya
MTAKUWWA awamu ya pili itakayotoa mikakati mahsusi ya kutokomeza aina
zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa miaka mitano
ijayo.”amesema Dkt.Gwajima
Kwa mujibu wa Dkt.Gwajima ,tathmini na Maandalizi ya MTAKUWWA II yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2022.
Akizungumzia
kuhusu uratibu na utekelezaji wa MTAKUWWA Waziri huyo alisema,Wizara
imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango huo kupitia maeneo nane ya
utekelezaji.
Amesema
mpango huo ambao utekelezaji wake ulianza Julai, 2017 na kutarajiwa
kufikia ukomo Juni mwaka huu, baadhi ya mafanikio yake ni Matukio ya
ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la
Polisi yamepungua kwa asilimia kutoka matukio 42,414 mwaka 2020 hadi
matukio 29,373 mwaka 2021.
Aidha,
matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yaliyoripotiwa kwenye Dawati
hilo yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15,870 mwaka 2020 hadi
matukio 11,499 mwaka 2021.
Dkt.Gwajima amesema,mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono ambavyo hadi Aprili 2022, jumla ya Vituo 21
vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) vimeanzishwa katika Hospitali mbalimbali za Serikali kwenye Mikoa 12 ikilinganishwa
na Vituo 14 vilivyoanzishwa hadi kufikia mwaka 2020/21.
Amesema,lengo
la vituo hivyo ni kuwezesha utoaji wa huduma hizo katika eneo moja ili
kuepusha usumbufu, ucheleweshaji wa huduma, kuharibu au kupoteza
ushahidi.
Waziri
huyo alisema,Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuratibu
uanzishwaji wa Vituo vya Mkono kwa Mkono katika Mikoa ambayo
haijaanzisha Vituo hivyo ikiwemo Mikoa ya Dodoma,
Singida, Tanga, Geita, Katavi, Rukwa, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mara, Kagera, Njombe, Songwe na Manyara.
“Vituo
hivi vinarahisisha huduma kwa kumpa fursa manusura kufika katika kituo
na kupata huduma za unasihi, utoaji taarifa kwa Afisa
wa
Polisi na kupata matibabu lakini pia vinarahisisha upatikanaji wa
haraka wa ushahidi unaotokana na vipimo vya kitabibu unaowasilishwa
katika Mahakama. “
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...