Na Janeth Raphael - Dodoma
WAZIRI wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewaonya Wakandarasi wote watakaohusika na ujenzi wa mkongo wa Taifa kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa ubora na umakini mkubwa na kuzingatia viwango vya ubora na yeyote atakayebainika kufanya vibaya atakuwa amejifungia kufanya kazi na Wizara na Serikali nzima.
Waziri Nape ametoa onyo hilo leo kwenye kikao kazi cha Wakandarasi kuhusu ujenzi wa kilomita 4,442 za mkongo huo wa Taifa, amesema kwa sasa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuhamishia shughuli zote za mkongo huo kwenye Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL).
Nnauye amewaambia Wakandarasi kuwa kama kuna kazi za kucheza nayo basi ni za Wizara nyingine, lakini sio Wizara ya habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa sababu itawafanya kukosa kazi za Wizara hiyo na Serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Inabidi maneno mengine magumu tuyaseme na kwenye hili itabidi niwe mkali kidogo…Kazi hii tunayoikamilisha Desemba 2022 itatuambia nani twende naye ili tusipasuane vichwa mbele ya safari,”Amesema Nnauye.
Aliongeza “Mimi siamini katika kumpiga mtu buti kabla ya kumwambia, mwambie kwanza, sasa imebidi niyaseme haya vizuri tumeweka fedha ya umma kwenye hii miradi lazima ifanyike kwa ubora na kwa wakati, kazi hii ya mbele ni kubwa zaidi na fursa zipo ila zitapimwa kwa kazi uliyopewa nyuma
Niwahakikishie mkifanya kazi vizuri mtafurahia kufanya kazi na sisi lakini mkifanya vibaya mtajutia kufanya kazi na sisi.”
Hata hivyo, Waziri huyo amesema kwa Mwaka 2022/23 Serikali inatarajia kujenga zaidi ya kilomita 1600 na vituo vipya 15 na lengo ni kufika Wilaya 81 na urefu wa kilomita 14,361 sawa na asilimia 95 ya lengo kubwa la kufikia kilomita 15,000 ifikapo Mwaka 2025.
“Kuna umuhimu kwa takwimu hizi kuwepo na ushirikiano wa SEKTA binafsi na serikali pekee haiwezi kumaliza, nitoe wito serikali ya awamu ya sita inaamini kwenye ushirikiano wa serikali na SEKTA binafsi katika kuendesha shughuli zake, yawezekana mmekutana na mawimbi mbalimbali niwahakikishie yametulia tupo tayari kushirikiana na mfanye kazi sawa sawa kwa kuwa mna mchango mkubwa kwenye maendeleo,”amesema.
Amesema tangu kuanza kujengwa kwa Mkongo huo mwaka 2009, ujenzi wake umefikia kilomita 8,319 na zaidi ya Sh.Bilioni 670 zimetumika na una vituo kwenye mikoa 25 Tanzania bara na Wilaya 43 kati ya 139 sawa na asilimia 30.9 zimefikiwa na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
“Mwaka 2021/22 zilitengwa Sh.Bilioni 170 kwa ajili ya kujenga kilomita 4,442 na kuongeza uwezo kutoka 200G kwenda 800G, jumla ya mikataba 22 ilisainiwa na ilihusisha kampuni nane, takwimu zinaonesha kati ya kampuni hizo sita ni za watanzania kazi hii inapaswa kuisha Desemba 2022, ikikamilika yote tutakuwa tumefikia kilomita 12, 761 kati ya 15,000 za lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025,”amesema.
Waziri Nape ameongeza kuwa mkongo ni muhimu katika kujenga uchumi wa kidigitali na kwamba serikali imeahidi itapitia baadhi ya sheria, sera na kanuni ili kujenga uchumi huo.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Jim Yonaz, amesema lengo la ujenzi wa mkongo huo ni kufikia kilomita 15,000 ifikapo Mwaka 2025 na unaoongoza Afrika Mashariki na Kati.
Akitoa taarifa ya mradi wa mkongo wa Taifa, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, ,Mlembwa Mnako amesema kuwa mkongo huo umesaidia kupunguza gharama za kusafirisha mawasiliano kwa njia ndefu ambapo awali walikuwa wakitumia satelaiti.
“Mwaka 2005 Serikali ilifanya uamuzi thabiti kwamba tuwe na mradi wa mkongo wa taifa na kati ya mwaka 2005 na 2007, ilifanyika tathmini ya mkongo uweje na kutafuta gharama za awali za kutekeleza mradi huu, na mwaka 2008 ambapo Serikali ilipata fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa benki ya Exim China,”alisema.
Pia amebainisha kuwa Mwaka 2009 mradi huo ulipoanza kutekelezwa zilijengwa kilomita 4,330 na ilifungwa mitambo yenye uwezo wa 10G na baada ya kipindi hicho Serikali ilitafuta fedha za kujengwa kilomita zingine 3,630 na hivyo kuwa na kilomita zaidi ya 7,000 zilizojengwa.
Amesema katika kikao hicho ni kwa ajili ya wakandarasi watakaojenga kilomita 4,442 za mkongo huo.
Mkurugenzi wa TTCL, Peter Ulanga, amesema shirika hilo limepewa jukumu la kuendesha na kuhudumia miundombinu ya mkongo huo na kwamba itahakikisha inaifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidigiti.
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza kwenye kikao kazi cha Wakandarasi kuhusu ujenzi wa kilomita 4,442 za mkongo wa taifa hii leo Jijini Dodoma .
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kushoto) na katibu mkuu wizara hiyo Jimmy Yonazi (kulia) kwenye kikao kazi cha Wakandarasi kuhusu ujenzi wa kilomita 4,442 za mkongo wa taifa hii leo Jijini Dodoma .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...