Na Pamela Mollel,Arusha
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, timu ya waendesha baiskeli wapatao 30 wanapanda mlima Meru ambao ni wa pili kwa urefu nchini.
“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa baiskeli kufika katika kilele cha mlima meru,” Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya biashara, wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Bakari Mnaya, alibainisha.
Mlima Meru una urefu wa Mita 4566 kutoka usawa wa bahari. Ni wa pili kwa urefu nchini baada ya Kilimanjaro.
Katika kuweka rekodi hiyo mpya katika sekta ya utalii, hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) imezindua utalii huu mpya wa kupanda Mlima Meru kwa kutumia baiskeli, ili kuleta tija zaidi kwenye sekta ya utalii nchini kwa kuongeza watalii na mapato.
Dk Mnaya aliongeza kuwa Hifadhi ya Arusha tayari ina mazingira mazuri na tofauti, hivyo kufikia hatua hiyo wanajipongeza kwa kuanzisha aina hiyo ya utalii na itaongeza wageni watakaofika nchini na mapato.
"Utalii huu katika hifadhi hii unakuwa wa pili baada ya Mlima Kilimanjaro kutumia utalii huu,ila lengo hasa kuvutia watalii zaidi wanaopenda kutumia usafiri huu,"alisema.
Aidha alisema pia zao hilo jipya ni maandalizi ya kukabiliana na wimbi la watalii wengi watakaokuja nchini kutokana na Filamu ya Royal Tour aliyotengeneza Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema katika safari yao watapita vituo vitatu wakitokea geti kuu la Momella ambavyo ni Miriakamba Hut, kituo cha pili ni Saddle Hut na siku ya tatu watafika kileleni katika mlima huo na kushuka.
"Kushuka ni rahisi hivyo watafika geti la Momella walipoanzia siku ya Jumanne ya Mei 10 mwaka huu,"alisema.
Alisema aina hiyo mpya ya utalii itaongeza wageni na kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza hifadhi na kuchangia pato la Taifa.
"Utalii unaofanyika wa kupanda baiskeli hivyo tumejiandaa kuweka usalama kwa wageni wetu pindi wanapopanda mlima huu,"alisema.
Afisa Uhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Catherine Mbena wa kitengo cha Mawasiliano, alisema wameanzisha utalii huo mpya, ili kuhakikisha watalii wanaokuja nchini wanapata ladha mpya kutokana aina ya tofauti za utalii.
Mratibu wa safari hiyo ya baiskeli kuelekea kilele cha Mlima Meru, Thad Peterson ambaye pia ni Mkurugenzi kampuni ya utalii ya Ndorobo, anasema Hifadhi ya Arusha haijawahi kuwa na baiskeli nyingi kama zinazoshiriki zoezi hilo sasa.
"Leo tuna wapanda baiskeli zaidi ya 27 ambao wamedhamiria kufika kileleni ili kuhamasisha aina hii mpya ya utalii wa kupanda mlima Meru Meru," alisema
Alishauri kupanda mlima huo ni muhimu kuwa na uzoefu na kuwa na baiskeli inayostahimili njia za porini ili kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tazama Africa, Jaffary Jah Malima, anaipongeza TANAPA na uongozi wa hifadhi hiyo kukubali kuanzisha aina hii mpya ya utalii ambao watachochea baiskeli kwa jumla kilometa 20, ikiwa ni kilometa 11 siku ya kwanza, kilometa 5 siku ya pili na kilometa 4 siku ya tatu na ya mwisho kufika kileleni.
"Utalii huu utaongeza ajira kwa baadhi ya watu na waongoza utalii pia tutaongeza mapato kwa serikali,"alisema.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya biashara,wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)Bakari Mnaya akizungumza katika uzinduzi wa aina mpya ya Utalii wa baskeli katika Hifadhi ya Arusha
Kamishna Mhifadhi wa Hifadhi ya Arusha Albert Mziray katika uzinduzi wa safari ya kwanza ya baskeli kupanda Mlima Meru
Mkurugenzi wa kampuni ya Tazama Africa,Jaffary Jah Malima aipongeza TANAPA nauongozi wa Hifadhi kwa kuanzisha aina mpya ya Utalii
Afisa Uhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)Catharine Mbena wa kitengo cha Mawasiliano akiwa katika uzinduzi wa aina mpya ya Utalii wa baskeli katika Hifadhi ya Arusha
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...