Na Jane Edward, Arusha
Kwa mara ya kwanza katika historia wilaya ya Ngorongoro halmashauri ya mji mdogo Loliondo Serikali kupitia shirika la umeme Tanzania Tanesco imewasha umeme wa Gridi ya Taifa baada ya kutumia umeme wa genereta kwa zaidi ya miaka 11 huku kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 kikitumika kwa mwaka kwaajili ya kununua mafuta ya diesel kuendeshea genereta hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Wilayani Ngorongoro,meneja wa shirika la umeme Tanesco Arusha, Mhandisi Herine Muhina amesema mradi huo wa umeme umetumia shilingi Bilioni 2.9 katika kukamilisha kuunganisha umeme Kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa 25,2021 na umekamilika Mei 4,2022 ikiwa ni takribani miezi Saba mpaka mradi huo kukamilika na kwamba kubwa zaidi ni nguzo za chuma zilizosimamishwa katika wilaya hiyo kwa mara ya kwanza Mkoani Arusha.
Amebainisha kuwa uwepo wa umeme huo wa uhakika utasaidia kupunguza gharama za mafuta ya diesel ambayo walikuwa wakitumia kuhakikisha wananchi hawakai giza na hivyo kulifanya shirika kutumia pesa nyingi ambapo kwa sasa wameokoa gharama hizo kwa kuwepo kwa umeme wa uhakika.
Amesema kuunganishwa kwa umeme wa Gridi ya Taifa katika wilaya hiyo kutachochea maendeleo kwa kufunguliwa viwanda,mahoteli ya kitalii pamoja na mambo mengine.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo la uwashaji umeme wa gridi ya Taifa amesema Tanesco imekuwa ikihakikisha inawapatia wananchi huduma bora katika upatikanaji wa nishati ya uhakika na kwamba zoezi hilo limekonga mioyo ya watu na ndiyo lengo la Serikali ya awamu ya sita.
"Tutaongea na wadau kuhakikisha eneo hili linakuwa na viwanda vya nyama ili kuwezesha wananchi kutokwenda mbali kutafuta masoko ya mifugo na kwamba umeme huo umekuja wakati muafaka" Alisema
Kwa upande wake msemaji wa Shirika la umeme Tanesco makao makuu Martine Mwambene amesema kwa muda mrefu kituo kimekuwa kikitumia mafuta ya genereta na kwamba shirika linaenda kuokoa pesa nyingi ambazo zitaelekezwa kwenye mambo mengine.
Amesema ipo Mikoa ambayo haijaingia Kwenye umeme kama Mkoa wa Kigoma na kwamba baada ya miaka michache ijayo Mkoa huo utakuwa na umeme wa gridi wa uhakika katika maeneo mbalimbali.
Amesema Wananchi sasa wanatakiwa kuwa sehemu ya miundombinu hiyo iliyowekwa na tanesco na kwamba kwa kufanya hivyo watasaidia miundombinu kutohujumiwa.
Picha ya eneo lililounganishwa umeme na Tanesco.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella akisalimiana na wadau wa Tanesco.
Msemaji wa Tanesco akifafanua jambo na wataalamu wa Tanesco Arusha.
Mfano wa nguzo za Chuma zilizotumika katika kuunganisha umeme gridi ya Taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...