Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara(TNBC)ameridhishwa na utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa 12 wa kusisitiza dhamira ya serikali kuendelea kuweka mazingira jumuishi na wezeshi ya kufanya biashara hapa nchini.
Akizungumza katika kikao cha Tamati Tendaji ya TNBC, Balozi Kattanga alisema wakati umefika kwa sekta za umma na binafsi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuleta matokeo chanya sambamba na kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kuifanya sekta binafsi iwe imara na yenye nguvu," alisema na kuongeza na kuongeza kuwa sekta za umma na binafsi lazima zifanye kazi kwa pamoja na kuaminiana.
Alisema kutekelezwa kwa mazimio ya Mkutano wa 12 wa Baraza ni ushaidi tosha kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mazingira yakufanya biashara yanaboreshwa ili kumfanya mwekezaji na mfanyabiashara avutiwe kufanya uwekezaji nchini.
“Hatua hii itatuwezesha kama serikali kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ambayo yatakwenda kuboresha huduma mbalimbali jamii na kufanya nchi kupiga hatua kimaendeleo,” alisema
Katika hatua nyingine Balozi Kattanga alisema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutengeza filamu ya Royal Tour inapaswa kuungwa mkono na wadau wote kwani matokeo chanya ya filamu hiyo yameanza kuonekana katika sekta za utalii na uwekezaji.
"Rais Samia Suluhu Hassan amejitoa kuitangaza Tanzania kimataifa.Tutegemee kupokea watalii wengi na wawekezaji hapa nchini," alisema.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC,Dkt.Godwill Wanga amesema baraza litaendelea kuratibu vikao hivi kutokea ngazi ya wilaya kwani ndipo changamoto zinapoibuliwa nakuletwa katika ngazi ya taifa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
“Napenda kuwaambia watanzania kuwa TNBC ipo kwaajili ya sekta binafsi na sekta za umma, katika maazimio tuliyopitisha katika kikao cha 12 tumefanikiwa kuyatekeleza kwa asilimia 85, tumeyafanya haya ili kuwapunguzia wafanyabiashara mzigo wa gharama kwa wafanyabiashara, ili sekta binafsi ziweze kukua pamoja na kuvutia wawekezaji” Alisema Dkt Godwill Wanga.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwa ni pamoja na kupunugza tozo na kusema jukumu lililopo ni kuhakikisha biashara zinaongezeka ili kuongeza mapato kupitia kodi mbalimbali.
Makanza amesema sekta binafsi imejipanga kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji katika masuala yanayohusu kujenga uchumi wa nchi.
“kwakweli tumeridhishwa na mrejesho wa utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita ambayo yametekelezwa kwa 85%, jambo hili limetujengea imani kwamba serikali imejipanga katika kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa na kunakuwa na uwajibikaji wenyentija katika masuala ya kujenga uchumi wa nchi” Alisema Paul Makanza.
Katika kikao hicho wajumbe walipongeza utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita kikiwa ni cha 12 yaliyotekelezwa kwa asilimia 85, ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa 13 utakaoongozwa na Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, akijadili jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Kamati tendaji ya Baraza hilo uliofanyika ikulu Jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 13 wa Baraza hilo ambao Mwenyekiti wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, (kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa kamati tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika ikulu Jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 13 wa Baraza hilo ambao mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kulia ni Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...