MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma (CCM), Mariam Ditopile amemtaka Waziri wa Nishati, January Makamba kuwa makini na Mradi wa Gesi Asili (LNG) uliokwama kwa zaidi ya miaka kumi.
Mradi huo wa LNG umekuwa ukisuasua na kuibua mjadala ndani na nje ya Bunge lakini akiwasilisha Bajeti ya Waziri wa Nishati, Makamba alisema mradi huo unatekelezwa katika eneo la Likong’o mkoani Lindi na unahusu usindikaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika Vitalu Na. 1, 2 na 4 katika kina kirefu cha bahari.
Alisema kazi zilizotekelezwa hadi kufikia Mei, 2022 ni pamoja na uwekaji nguzo za alama katika eneo la mradi; ujenzi wa barabara kuzunguka eneo la mradi, kuendelea na stadi za kisayansi (geoscience) na stadi za mitambo itakayosimikwa katika eneo la mradi.
Pia, kuendelea kuboreshwa kwa nyenzo zinazotumika katika majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) kati ya Serikali na wawekezaji; kupatikana kwa Mshauri Mwelekezi ambaye anaishauri Serikali kuhusu masuala ya ufundi, sheria, fedha, biashara na uchumi; na kuendelea na majadiliano ya Mkataba wa HGA kati ya Serikali na Wawekezaji.
Akichangia bajeti hiyo leo Alhamisi tarehe 2 Juni 2022, Dipotile amesema, “Waziri Makamba ukitulia kwenye mradi wa LNG unakwenda kuacha historia kwenye mradi huu. Mfupa huu umeshindikana kwa zaidi ya miaka 10 na mimi naomba uangalie jirani zetu Msumbiji anahangaika kwenye suala la usalama, neema inaambatana na hofu ya usalama, nenda kalifanye hili na lianze kutekelezwa.”
Katika mchango wake, Ditopile amesema, “January Makamba namfahamu vizuri tangu nimepata ufahamu wa akili na kama hammujui ndiye kijana alihusika kuandika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM 2015-2020 iliyotuletea ushindi mkubwa wa kihistoria katika uchaguzi mkuu 2020.”
“Huyu January Makamba alipata nafasi kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira, wanasema mzigo mzito mpe mnyamwezi lakini mzigo mzito alipewa Msambaa na akauvusha, alipewa mzigo wa kwenda kufuta viroba na mifuko ya plastiki na aliweza, sina mashaka na weledi wake,” amesema
Amesema nimefuatilia mjadala, kila mbunge anakusifia (January Makamba) na tayari wamekuelewa na wanakwenda kupitisha bajeti hii ya nishati kama kipimo, sisi tunakukopesha imani yetu na kaitendee mema sekta ya nishati"
“Waziri Makamba ametuletea bajeti kama ya ‘action road map’ katika kufikia maono ya wizara. Umetupa mpaka kipaumbele na mawazo mapya utakavyoihusisha sekta binafsi na jinsi utakavyopata fedha kuendesha mashirika yao. Nakupongeza sana,” amesema
Aidha, Ditopile amesema, shida kubwa ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) “ni kukatika kwa umeme, pamoja na huduma mnayotoa mnapaswa kujua umeme ukikatika mtumiaji anatafuta kwingine, kipindi ukikatika Tanesco inapoteza mapato na CAG anapaswa kukagua kipindi hicho unapokatika ni kiasi gani mnapoteza mapato.”
“Lazima TANESCO muende na teknolojia, mnapokwenda kubadili nguzo na nyanya lazima mkate umeme. Leo Dar es Salaam mnabadili nguzo kutoka za miti kwenda za zege mnakata umeme, kwa hiyo mnaweza kuwa na mbinu mbadala kufanya mabadiliko hayo pasina kukata umeme,” amesema
Transfoma
Vilevile, Ditopile ameishauri wizara hiyo kuhakikisha umeme ambao umefika vijijini haujafika vitongojini, “tuangalie maeneo ambayo hayajafika kwenye baadhi ya maeneo.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...